Wednesday, May 18, 2005

Sakata la CITY water

Nakuambia mambo yameiva. Hawa jamaa wa city water nani kakuambia watakubali kirahisi? Wamesema wataenda mahakamani. Nakuhakikishia hii mambo itakuwa kama yale ya TTCL. Si mnakumbuka ilianza hivi hivi kama utani. Jamaa wakagoma kutoa pesa zilizobaki. Songombingo za kisheria zikaanza. Jamaa wakavimba mahakama zote mpaka ughaibuni wakaibuka washindi. Sasa hivi wanajimwaga bado. Nasikia wataongezewa tena mkataba. Nakuapia wadanganyika tutakoma kipindi hiki. Unajua kuna watu ukiwaambia kuna wazungu matapeli watakumaliza. Watakuambia hapana, mzungu hawezi kuwa tapeli, atakuwaje tapeli wakati wao ndio magwiji na wapiga debe wa utawala bora? Hapo ndio tunapodanganywa. Tusipojihadhari tutapigwa bao lingine.

Daktari azidi kubanwa

Yule Daktari mjerumani anayepinga matumizi ya dawa za makampuni ya kibeberu na kusisitiza matumizi ya vitamini amezuiwa na mahakama huko Berlin kuendelea kutangaza kwa kijerumani kwamba vitamini zake zina uwezo wa kutibu kansa la sivyo atatozwa faini ya EURO 250,000. Hatua hiyo inafuatia kugundulika kwamba kijana mmoja kwa jina la Dominik Feld mwenye umri wa miaka tisa alikufa baada ya kuanza kutumia vitamini za Dr. Rath na kusimamisha tiba ya kansa aliyokuwa akiendelea nayo. Mambo yanazidi kuwa moto. Mambo ya kufanyika maabara sasa yamegeuka ukumbi wa mabishano kama siasa. Nitazidi kuwafahamisha maendeleo ya mkasa huu.

Kumbukumbu ya Mwanaharakati Malcom X

Wiki hii huko New York kuna maonyesho ya shujaa Malcom X. Soma habari hiyo hapa

Monday, May 16, 2005

Umoja Wa mataifa wamkemea Daktari

Yule Daktari niliyewaambia anapinga dawa za kuongeza maisha kwa waathirika wa UKIMWI na badala yake kusisitiza vitamini amepigwa mkwara na umoja wa mataifa. Nimepata hii habari toka kwenye mlolongo fulani wa barua pepe sijuhi ilitoka kwenye chombo gani cha habari. Naiweka hapa ili muisome.

Makala Mpya

Nimeweka makala mpya inayoitwa kasi ya ahadi za ajira. Bonyeza hapa uisome. Makala nyingine zipo kwenye kona yangu ya makala.

Hivi Angola inauza wapi mafuta yake?

Afrika kweli kiboko. Mimi najiuliza ni wapi Angola inauza mafuta yake? Hii ni nchi ya SADC lakini sijuhi kama kuna nchi inayonunua mafuta toka Angola. Wengi wanaagiza uarabuni. Jumuiya kama SADC inafanya nini sijuhi kupunguza hali hii ya utegemezi wa kununua bidhaa zinazopatikana kwenye moja ya nchi za jumuiya toka nchi za mbali. Na usione ajabu Angola ikawa inaagiza mafuta toka nje kama inavyofanya Nigeria. Inauza Mafuta ghafi halafu inanunua yaliyosafishwa. Kweli safari ya Afrika bado ni ndefu!!

Saturday, May 14, 2005

Vita dhidi ya dawa za kurefusha maisha

Kuna malumbano makali Afrika ya Kusini baada ya kundi la wanaharakati wanaounga mkono matumizi ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa UKIMWI kupeleka kesi mahakamani kutaka Daktari wa Kijerumami Matthias Rath aache kupinga matumizi ya dawa hizo. Daktari huyu amekuwa mpinzani mkubwa wa ARV's kwa madai kwamba zina madhara makubwa sana kiafya. Badala yake anapendekeza lishe bora pamoja na matumizi ya vitamini muhimu kwa waathirika. Kesi ilipotajwa jana kulikuwa na makundi mawili, moja likimuunga mkono daktari huyu na lingine likimpinga. Nusura zipigwe nakuambia. Dr. Rath anasema kwamba madawa haya si chochote bali ni kuendeleza biashara ya makampuni makubwa ya dawa duniani. Unaweza kutembelea tovuti yake kwa kubonyeza hapa

City Water

Soma habari hii hapa uone jinsi hawa "wenzetu" wawekezaji wanavyofanya. Habari za hawa jamaa kwamba walikuwa hawana chochote zilisemwa siku nyingi sana lakini kama kawaida waliosema wakaanza kupigwa mabomu na viongozi. Wakaambiwa si wavumilivu. Wakaambiwa kampuni yenyewe ndio kwanza imeanza kazi lakini watanzania wanataka mabadiliko haraka sana. Wakaambiwa subirini. Sasa sijuhi wataombwa radhi wale waliokuwa wanasema ukweli kwamba hao jamaa hawataweza kufanya lolote au vipi? Wamesubiri na maneno yao yamethibitika. Wakati mwingine viongozi wajifunze kusikiliza pia sio kutoa maagizo na vitisho tuu kwa watu wenye mawazo na maoni tofauti.

Baba Moi Mjanja mwenzao

Nasikia kati ya mambo ambayo rais mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi ameyafanya ni pamoja na kujenga chuo kikuu katika shamba lake kubwa huko Turkana. Chuo hicho kwa mujibu wa taarifa nilizonazo kina wanafunzi karibia mia tatu. Hii kwa mtazamo wangu ni kitu kizuri zaidi kuliko wanavyofanya viongozi wengi wa Afrika kuweka fedha zao katika mabenki ya Uswisi au nchi nyingine za magharibi. Angalau zikiwekezwa nchini zinaweza kufaidisha wananchi.

Wednesday, May 11, 2005

Uwezo wa kuhoji

Watu wanapokuwa wamebanwa kisawasawa, wanakuwa wanafikiria tuu namna ya kupata chakula cha leo. Si kesho wala keshokutwa. Si Elimu wala chochote kingine. Ni chakula kwanza. Utafikiriaje chochote wakati njaa imefanya makao makuu kwenye tumbo lako? Hii ndiyo hali halisi inayowakabili watanzania wengi na hasa vijana. Hali ya ajira ni mbaya sana. Vijijini hakukaliki. Wakati mwingine tunawalaumu watanzania kwamba ni wavivu. Kama ukitaka kujua si wavivu kiasi cha kutisha, safiri kuanzia Tunduma mpaka Dar-es-Salaam, ona mazao yalivyopangwa barabarani kwa bei ya kutisha. Nina maana bei ndogo kabisa. Nenda Shoprite (kama Si Shopwrong) uone vitunguu na nyanya toka "bondeni" ambavyo vimekuzwa kimaajabu. Kwa ufupi ni kwamba mazingira ya vijijini hayavutii kukaa. Mimi nina imani kubwa sana hakuna kijana atakayekubali kuja kuhangaika siku nzima mjini akiuza shati moja kama angeweza kulima nyanya zake na zikamrudishia fedha zake. Kijana kama huyu anayefikiria chakula cha leo hawezi kuhoji mgombea anayemwambia atampatia ajira. Anachoangalia ni lini tarehe 30 oktoba itafika akapige kura ili mgombea apite na apate ajira. Kwamba itapatikanaje hataki kuhoji, hata nguvu za kuhoji hana. Angekuwa na uwezo angesogeza kalenda mbele ili Oktoba ifike mapema apate ajira yake. Kwake hajuhi hata kama mgombea ana mpango kabambe wa kuongeza ajira itamchukua muda mrefu kabla huo mpango kabambe haujafanikiwa. Kama ni kuanzisha viwanda itabidi vijengwe (Sitaki kuingia ndani sana hapa, naanzia tuu kwenye ujenzi), vikamilike vianze uzalishaji. Vyovyote vile ni lazima kutakuwa na maandalizi yatakayochukua muda mpaka ajira izalishwe. Ukweli huu ndio hao vijana watatakiwa waujue.

Tuesday, May 10, 2005

Ripoti ya kumaliza matatizo ya Afrika

Bonyeza hapa usome hii ripoti ambayo "itamaliza matatizo yote ya Afrika". Blair kaamua kuyamaliza ndugu zangu. Nasikia anatupenda kweli waafrika.

Mjadala wa Mama Kibaki

Wale ambao wanapenda kutoa maoni yao kuhusu mama Kibaki na hasira zake wanaweza kuyatoa hapa

Monday, May 09, 2005

Makala mbili

Nimeweka makala mbili nilizoandika. Moja inaitwa utamaduni wa amani. Isome kwa kubonyeza hapa na nyingine inaitwa habari za udaku. Isome hapa

Angalieni hawa Wabeligiji jamani.

Angalieni hawa Wabeligiji HAPA yasije yakatufika kwani na sisi huwa ni mabingwa wa kuiga.

Demokrasia na Mkumbokrasia

Hivi kweli wengi ndio Demokrasia? Nadhani kuna Demokrasia na Mkumbokrasia(Mobcracy). Kuna mtu leo ukimuuliza kwa nini anamshabikia mgombea fulani wa kiti cha urais hawezi kukupa sababu. Mwingine haelewi hata huyo anayemshabikia ana ajenda gani. Kuna msemo unazungumzwa sana sasa hivi- huyu ana mvuto. Muulize sasa mvuto kwa nini? Hapo ni heri umchape fimbo sita kuliko akupe jibu kwa sababu atakuwa hana. Kama wapiga kura wengi wanafuata mkumbo kutakuwa hakuna Demokrasia bali ni Mkumbokrasia.

Upofu wa Rangi

Kuna mjadala mzuri sana unaoendelea Afrika ya Kusini. Mjadala huu unauliza swali; je watu wa Afrika ya Kusini wanakuwa vipofu wa rangi tangu kukoma kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994? Upofu wa rangi hapa unatumika kuuliza swali ikiwa watu wamepunguza kubaguana kutokana na rangi zao. Mjadala ni mzuri sana. Wengine wanasema kuna maendeleo katika hilo, wengine wanasema hali bado si nzuri. Wanaosema mambo yamebadilika wanaangalia hoja kama vile weusi kupata kazi za ngazi ya juu, wengine wanasema yeyote anaruhusiwa kuwa mahali popote. Wanaosema mambo bado wanatoa hoja kama vile watu weupe kupinga kwa nguvu zote kitendo cha serikali kubadilisha majina ya baadhi ya miji au mitaa. Kilichovutia zaidi ni onyo lililotolewa kwamba katika hatua za kusaidia weusi, lazima wazungu wasianze kubaguliwa tena. Ukajaribu kurekebisha matatizo ya ubaguzi siku za nyuma ukazalisha ubaguzi mwingine. Hili ni muhimu pengine si kwa rangi tuu. Katika mazingira ya nchi nyingine ambapo ubaguzi wa rangi si wa msingi sana, kuna hatua za makusudi za kupunguza ubaguzi wa kijinsia kwa mfano. Pamoja na umuhimu huu hatua hizo zisizalishe tabaka jingine nyonge katika jamii- ni lazima kuwepo na mizania. Mwalimu Nyerere wakati fulani alisema kwamba jitihada za kupigana na ubaguzi wa rangi zilipofanikiwa ziliwasaidia si tuu weusi bali pia weupe waliokuwa wakiathiriwa na mfumo huo. Si weupe wote waliokuwa na hali nzuri chini ya mfumo wa kibaguzi.

Sunday, May 08, 2005

Sadaka na Rambirambi

Soma habari ya mchanganyiko wa sadaka na rambirambi hapa

Dawa za kulevya zinabwiwa mchana kweupe Dar

Soma habari hii ya kusikitisha hapa uone jinsi vijana wanavyoharibiwa na dawa za kulevya. Mtaalam Profesa Kilonzo anaona jamii nzima ina cha kufanya kwa hili; wazazi, vyombo vya sheria, vyombo vya dola na vijana wenyewe.

Saturday, May 07, 2005

Kupokea kwa kishindo

"Au kama wanaompokea wana kazi, basi kiongozi huyo ajue kuwa shughuli za uzalishaji katika taifa lenye matajiri asilimia moja na masikini asilimia 99 zimesimama". Hii ni nukuu toka kwa msomaji wa blogu hii kufuatia kale katabia nilikokemea cha viongozi kupokelewa kwa kishindo. Nakubaliana naye moja kwa moja sina ubishi na hili.

Msome Mzee Wa Kiraracha

"Bw. Mrema akasema ni rahisi Osama kupatikana, kuliko Kikwete kupenyeza mabadiliko katikati ya vigogo wa CCM. ?Ili Kikwete awe mnyama msafi, kwanza anatakiwa akaushe tope la CCM, kwa kukifumua Chama hicho na kukisuka upya. Kuondoa wachafu wote ambao wamekula tangu uhuru, hapo kidogo ataona mwanga, vinginevyo, atakuwa anajisumbua" . Msome zaidi hapa. Usisahau kwamba huyu pia ni mzee wa ruzuku.

Wapinzani Igeni kwa Howard

Bwana Michael Howard Kiongozi wa Chama cha Conservative huko Uingereza anaachia uongozi ili kumpisha mtu mwingine kuongoza chama hicho. Baada ya jitihada zake za kurudisha chama chake madarakani kushindwa kwa mara mbili mfululizo kaamua kujitoa nje licha ya safari hii kufanya vizuri ikilinganishwa na wakati wa uchaguzi uliopita. Wale wagombea urais wa maisha wa upande wa upinzani Tanzania anaowasema Macha nadhani wamemsikia. Tunatarajia watajifunza toka kwake. Soma habari hiyo hapa

Uchaguzi wa kihstoria

"Katibu wa Msikiti wa Mtambani, Sheikh Abdallah Ally alisema uchaguzi wa safari hii utakuwa ni wa kihistoria kwa sababu itakuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi wa ngazi ya juu serikalini wote kuwa Waislamu. "Yaani Rais Mwislamu, Makamu wake Mwislamu na Rais wa Zanzibar Mwislamu. Katika awamu zilizopita ilikuwa haijawahi kutokea hivyo. Hii itafuta ile dhana kwamba Waislamu hawana elimu," alisema Sheikh Ally". Soma mawazo ya Sheikh huyu zaidi hapa

Friday, May 06, 2005

Wananchi na kuwapokea viongozi

Hivi tutaacha lini hii tabia ya kuwaambia watu waache kazi zao kwenda kupokea viongozi? Hii ni dalili mbaya lakini sijuhi kama inamwonyesha kiongozi kwamba kuna mzigo mkubwa unaomkabili. Sijuhi kama mtu mwenye shughuli yake ya maana ya kufanya ataicha na kwenda kukaa barabarani kumlaki kiongozi. Kiongozi anapaswa ajue kwamba akiona umati mkubwa sana aelewe wengi wao hawana shughuli ya kufanya. Badala ya kufurahi na kushangilia kwamba amepokelewa kwa kishindo ajue ana mzigo wa hawa ndugu- nina maana mzigo wa kuzalisha kazi za kufanya. Wengi wa wapokeaji hao bila shaka ni vijana (sina maana ya vijana wenye umri wamiaka 50 na kuendelea). Hili ni kundi ambalo limeathirika sana kwa kukosa shughuli ya kufanya. Kiongozi mwenye mtizamo mpana asifuraie kupokewa kwa kishindo, aione hiyo kama changamoto mbele yake. Aone kwamba watu wanaompokea, kumsikiliza na kumpamba siku nzima asilimia kubwa hawana cha kufanya. Wenye cha kufanya wako kwenye shughuli zao. Cha muhimu zaidi na zaidi ni kutowalazimisha watoto wadogo washiriki katika mapokezi kama hayo.

Thursday, May 05, 2005

Ujana na Urais

Kwa kweli kabla hujafa hujaumbika. Kijana anakuwa na miaka 55? Hiyo ni kali zaidi. Naambiwa mwenyekiti wa CCM katika hotuba yake ya mkutano mkuu wa kumtafuta mgombea alitoa wito kwamba ateuliwe mtu kijana. Angetoka wapi wakati hakuwepo kijana kwenye jopo hilo? Hata lile la watu 11 hakuwepo. Kuna watu wanaosema kwamba hotuba ya Mwenyekiti huyo imemsaidia mshindi. Wenye mtazamo huo wanakubali kwamba ni KIJANA. Kijana miaka 55? Hiyo ni definition mpya sana ya CCM. Lakini imekuwepo muda mrefu sana. Sasa hivi wastani wa muda wa kuishi kwa mtanzania ni kama miaka 46 sasa hapo ina maana kwamba hata umri wa wazee na vijana upangwe upya. Hata umri wa kustaafu kazini upunguzwe pengine uwe miaka 50. Umri wa kugombea urais kikatiba inabidi upunguzwe pia. Kila kitu kinabidi kirekebishwe kulingana na umri mpya wa kuishi kwa sababu hakuna matarajio kwamba siku za karibuni wastani huo utapanda.

Wednesday, May 04, 2005

Kutawala kwa zamu

Kuna wakati Macha alipendekeza njia za kumpata rais. Kati ya hizo ni kuwa na rais mwislamu na Mkristo kwa sababu watu wa dini hizi mbili wameshika bango sana. Nyingine ilikuwa ni Kumomba George Kichaka atusaidie kama anavyosaidia Iraq na Afrighanistan na nyingine ambazo hazitangazwi lakini ziko chini ya uangalizi wake. Mimi napendekeza utawala kwa zamu. Kwa vile rais anaweza kuongoza kwa miaka kumi basi ni rahisi sana hawa jamaa wote waliojitokeza kupitia CCM wakaongoza kwa zamu yaani mwaka mmoja mmoja watakachokubaliana tuu ni kuondoa "Outlier". Yule wa kumi na moja aondolewe kwa kigezo cha umri. Mwenye umri kubwa aombwe akapumzike kijijini kwake kwa amani, waliobaki watawale kwa mwaka mmoja mmoja. Hii itasaidia sana "kuimarisha mshikamno" wa chama twawala. Rais akichaguliwa ahakikishe anashawishi bunge kubadili katiba ili staili hii mpya ikubalike

Tuesday, May 03, 2005

Asilimia kumi, Rushwa na Sadaka

Umeshawahi kujiuliza uhusiano kati ya asilimia kumi, rushwa na sadaka? Swali hili linanitatiza sana kwani tunaambiwa Bwana Mungu wa Ibrahim, Yakobo na Isaka alisema tumtolee asilimia kumi ya pato letu. Upande mwingine tunaambiwa kwamba rushwa mara nyingi huwekwa katika kiwango cha asilimia kumi ya gharama halisi ya pato utakalopata. Kwenye mfumo wa rushwa,iIli kupata tenda tunaambiwa kwamba unahitajika uwape watoa tenda asilimia kumi. Kuna uhusiano wowote au ni hisia zangu tuu?
Sadaka mimi bado sijaweza kuielewa vizuri. Muumba wa mbingu na nchi na vyote vilivyomo anaitaji kweli visenti vyako? Kama anavihitaji basi asilimia kumi ni lazima iwe baada ya kutoa matumizi yako. Hivyo kama unapata laki moja, basi utoe kodi ya nyumba, chakula, usafiri, ada ya watoto, matibabu nakadhalika. Kitakachobaki toa asilimia kumi mpe muumba.

Ni kuongoza tuu?

Nimekuwa najiuliza swali hili kila mara. Hivi watu wanavyogombea uongozi nia yao huwa ni kuongoza tuu? Nilianza kujiuliza swali hili zamani sana. Sielekei sana kugundua sababu hasa ya hata mtu kwenda "kwa Babu" kutafuta uongozi. Hivi kuongoza tuu watu unakutolea macho hivyo? Nadhani sababu ni nyingi mno. Kuongoza ni kajisehemu kadogo sana ka sababu hizo. Sidhani kama utaenda kwa babu ili tuu uongoze watu. Watu wanapenda ujiko bwana. Kutambulika. Kuitwa mheshimiwa badala ya ndugu fulani. Kuna wakati bunge lilipoteza muda wa wapiga kura wao mwingi wakijadili kwamba sasa waitwe waheshimiwa na si ndugu au bwana au bi au bibi. Ni lazima watofautishwe na wengine. Sijuhi ni mpiga kura gani aliwatuma kwenda kujadili hayo mambo. Uheshimiwa unakuja tuu hata bila kuutungia kanuni. Timiza wajibu wako, fanya kazi kwa bidii. Toa mchango kwa jamii yako (si mchango wa harusi) mchango wa maendeleo- simanishi pesa hapa. Mawazo, kukusanya rasilimali watu zilizopo katika jamii, tambua uwezo wao, weka mawazo yao pamoja, buni mkakati wa maendeleo pamoja. Baada ya hapo utaona utaitwa mheshimiwa sana. Hutahitaji kwenda kujadili bungeni utambuliweje. Uchaguzi wa urais ndio huo. Watu nasikia wanachafuana vibaya sana. Wanapigana vikumbo. Wanapigania nafasi moja ambayo itakuja tena baada ya miaka kumi. Wanataka kuongoza watanzania. Je ni kuongoza tuu? Ni maslahi binafsi? ni kuitwa mheshimiwa, mtukufu mpendwa wetu rais........ Ni ving'ora vya kutishia wananchi wako na kusafirishwa kwa mwendo wa kasi kama vile unatorishwa au? Lazima tuwaulize hawa jamaa swali hili: Kwa nini unataka kuwa rais? Ukishapata jibu muulize kwa nini utumie sana nguvu, uchafu, matambiko na mambo mengine ya ajabu? Kuna la zaidi si kuongoza tuu.

Mke wa Kibaki katoa mpya

Mama Kibaki katoa Mpya. Bonyeza hapa

Ulaya Mwaendafanyani?

Kuna majigambo kwamba huduma za afya zimeimarishwa sana Tanzania sasa hivi. Kwa kiasi gani si ngumu kuelewa. Kama huduma zingekuwa nzuri na za kuridhisha tusingeona wazito wakihaha kwenda ulaya na Afrika Kusini kutibiwa magojwa yanayotibika hapo kwetu. Kama kweli huduma zimeimarika Ulaya mwaendafanyani? Nauliza. Tukutane wote Muhimbili basi ili kieleweke kwamba mambo ni barabara.

Hodi hodi

Naingia kwenye ukumbi wa blogu kwa kuwaambia watu- Amka kumekucha. Muda wa kuanza kubadilika kifikira ndio huu japo tumechelewa. Blogu hii itakuwa inahamasisha fikra mpya. Kuamsha mijadala. Jadili bila jazba. Toa maoni bila kuogopa kupingwa. Tutapingana pasi na kupigana. Tutapigana kimawazo na sio kwa ngumi, mapanga na bunduki. Tutaanza na hoja ya utamaduni wa amani. Tutaujengaje? Hoja zijadiliwe bila jazba. Naingia sasa ukumbini

Utamaduni wa kuambiana Ukweli

Ukifuatilia matatizo yanayotokea Togo sasa hivi utagundua kwamba yamechangiwa na utamaduni wa waafrika wa kutotaka kuambiana ukweli. Wakati Eyadema mzee alipofariki Febuari mwaka huu na Mwanaye Faure kumrithi kusivyo halali, Jumuiya ya ECOWAS iliingilia kati kuataka kutatua mgogoro huo lakini ikautatua kwa kutoambiana ukweli. Baadhi ya watu waliwasifu sana ECOWAS kwa kumlazimisha Faure aondoke madarakani na baadhi wakaanza kuilaumu sana SADC kwamba imeshindwa kumlazimisha Mugabe aondoke madarakani. Hawa niliwaambia kwamba hakuna suluhisho la kudumu kwa Togo kwa kuwa Faure atakuja madarakani kwa kile kinachoitwa "uchaguzi wa kidemokrasia". Walichosahau ni kwamba Watogo wamechoshwa na jina la Eyadema kwa njia ya uchaguzi au kijeshi au vyovyote vile. Baba katawala kwa zaidi ya miongo mitatu, mwanaye naye sasa atatawala kwa miaka kadhaa kwani bado ni kijana-ana miaka 39 tuu. Baadaye nikaangalia kipindi cha "Hard Talk" cha BBC kilichoendeshwa na Lyce Docet akimhoji katibu mtendaji wa ECOWAS, kati ya mambo mwanadada huyu aliyombana nayo katibu huyu ni tetesi kwamba baada ya mazungumzo ya kumtaka Faure aondoke madarakani na yeye kuonekana kukataa, ECOWAS walimhakikishia kwamba angerudi madarakani kwa njia ya uchaguzi. Ndipo bwana huyu akakubali kuachia madaraka ya kupora. Kama tetesi hizi ni kweli basi ECOWAS inawajibika pia kwa matatizo yanayotokea Togo na yatakayozidi kutokea kwa kutosema ukweli kwamba watu wamelichoka jina la Eyadema. Hili ndio tatizo la kutoambiana ukweli. Tujenge utamaduni wa kuambiana ukweli hasa kwenye siasa.


KITABU CHA WAGENI