Monday, May 09, 2005

Upofu wa Rangi

Kuna mjadala mzuri sana unaoendelea Afrika ya Kusini. Mjadala huu unauliza swali; je watu wa Afrika ya Kusini wanakuwa vipofu wa rangi tangu kukoma kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994? Upofu wa rangi hapa unatumika kuuliza swali ikiwa watu wamepunguza kubaguana kutokana na rangi zao. Mjadala ni mzuri sana. Wengine wanasema kuna maendeleo katika hilo, wengine wanasema hali bado si nzuri. Wanaosema mambo yamebadilika wanaangalia hoja kama vile weusi kupata kazi za ngazi ya juu, wengine wanasema yeyote anaruhusiwa kuwa mahali popote. Wanaosema mambo bado wanatoa hoja kama vile watu weupe kupinga kwa nguvu zote kitendo cha serikali kubadilisha majina ya baadhi ya miji au mitaa. Kilichovutia zaidi ni onyo lililotolewa kwamba katika hatua za kusaidia weusi, lazima wazungu wasianze kubaguliwa tena. Ukajaribu kurekebisha matatizo ya ubaguzi siku za nyuma ukazalisha ubaguzi mwingine. Hili ni muhimu pengine si kwa rangi tuu. Katika mazingira ya nchi nyingine ambapo ubaguzi wa rangi si wa msingi sana, kuna hatua za makusudi za kupunguza ubaguzi wa kijinsia kwa mfano. Pamoja na umuhimu huu hatua hizo zisizalishe tabaka jingine nyonge katika jamii- ni lazima kuwepo na mizania. Mwalimu Nyerere wakati fulani alisema kwamba jitihada za kupigana na ubaguzi wa rangi zilipofanikiwa ziliwasaidia si tuu weusi bali pia weupe waliokuwa wakiathiriwa na mfumo huo. Si weupe wote waliokuwa na hali nzuri chini ya mfumo wa kibaguzi.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI