Friday, July 22, 2005

Mambo ya blogu

Leo Ethan alitoa shule kuhusu "Community Blogging". Lilikuwa somo la nguvu sana. Washiriki walikuwa na furaha na wengi wamehamasika kuanzisha blogu zao na kuanzisha jamii yao ya mtandao wa blogu. Mimi nilizungumzia kidogo kuhusu blogu za Kiswahili; tunaandika nini, ni nani wanaandika nakadhalika. Wengi walifurahia jinsi ambavyo watanzania wanachipukia katika ulimwengu huu wa blogu na jinsi ambavyo wengi wetu tunavyojadili mambo yahusiyo nchi yetu, na ulimwengu kwa jumla kinyume na baadhi ya wanablogu wa nchi nyingine ambao huzungumzia mambo yao binafsi, familia na rafiki zao. Changamoto kubwa waliyotupa ni je ni nani anasoma tunayoaandika? Tutahakikishaje kwamba mawazo yetu yanasomwa na watu wengi zaidi? Hili ni jambo la msingi na inabidi wanablogu wote tubunge bongo kuhakikisha tunasomwa na watu wengi zaidi hasa wale ambao hawana "internet". Tujadiliane kwa hili kurahisha ufikishaji wa ujumbe kwa jamii. Lazima nikiri kwamba Ethan ni mtu muungwana, mpenda mijadala na mhamasishaji mzuri anayeweza kukufanya ukawa na blogu hata kama ulikuwa huna mpango wa kuwa nayo. Anaijua Tanzania kiasi pia, ameniambia ameshakuwa Dar mara kadhaa na ametembelea Zanzibar na Mikumi. Tuongeze bidii sauti zetu zitasikika.

Thursday, July 21, 2005

Nimekutana na Ethan Zuckerman

Leo jioni nimekutana na Ethan Zuckerman Tumejadili mambo kadhaa likiwepo jambo muhimu la wanablogu wa Tanzania. Jambo moja analosema ni kwamba watanzania wengi wenye kublogu ni waandishi na wamejikita sana kwenye mijadala ya kisiasa. Si kwamba ni vibaya. Jingine ni kwamba watu wengine mitaani hawako kwenye hii taaluma ya kutumia blogu. Hili la pili lina maelezo- miundombinu hafifu; si rahisi kwa watu wengi kutumia blogu kutoa mawazo yao kwa vile teknolojia bado ni ya hali ya chini. Jingine la msingi ni kwamba je ni watu wangapi wanaosoma mawazo yetu tunayoandika kwenye blogu? Kama wasomaji ni wachache ni namna gani basi tunahakikisha kwamba mawazo yetu yanafikia jamii kupitia magazeti na vyombo vingine? Hili ni jambo la kufikiria kabisa wanablogu wote watanzania. Mambo tunayoandika kwenye blogu yanawafikia wanajamii? Kwa mfano wanasiasa kweli wanasoma blogu? Kama hawasomi tutawafikishiaje ujumbe? Kaniuliza pia jambo lingine ambalo sikuwa na jibu lake. Hili waandishi mnaweza kulijibu. Ni kweli kwamba mnayoaandika kwenye blogu hamyaandiki kwenye vyombo vya habari mnavyofanyia kazi? Kwa kuwa siandiki magazetini sikuwa na jibu. Labda msaidie hapo.
Kesho atatoa mhadhara hapa chuoni nitahudhuria na kutoa mchango wangu kuhusu blogu za kiswahili.

Saturday, July 16, 2005

Ugaidi

Kwa nini hawa watu wanaoitwa magaidi watoke Misri, Saudi Arabia, Pakistan na nchi nyingine zenye uhusiano mzuri na Marekani na Uingereza? Kwa nini hawatoki nchi kama Iran au Iraq(kabla ya kuvamiwa)? Hili jambo limekuwa likinitatiza mno lakini naanza sasa kupata Mwanga. Huu urafiki wa baadhi ya nchi za kiarabu na nchi za magharibi hauungwi mkono na watu, ni urafiki wa viongozi hivyo wanajaribu kuonyesha hisia zao kwa njia hizi ambazo nchi za magharibi zinaita ugaidi. Lakini kuvamia Iraq na kuua hovyo si ugaid hata kidogo, ni ukombozi. Kabla ya kuvamiwa Iraq kulikuwa hakuna kitu kama watoa maisha mhanga. Naam, sasa wamezalishwa wa kutosha. Kulikuwa hakuna ushahidi wowote wa Alkaida na Iraq. Naam sasa wana tawi kabisa. Kwa vile wanataka Iraq iwe na uhusiano na nchi za magharibi sasa wananchi hawataki wanaonyesha kwa vitendo kama vya kujitolea mhanga, hali ambayo haikuwepo siku za nyuma.
Kwa wale wasikilizaji wa BBC nadhani mmesikai mjadala alioendesha Tido Mhando katika kipindi cha wiki hii- Jumamosi, tarehe 16/07/2005, mmoja wa washiriki wa mjadala ameongea jambo la msingi sana. Kwamba ni waafrika wangapi wanakufa kwa kuchinjwa, wanakufaa kwa njaa, magonjwa yanayotibika nakadhalika kila leo? Hakuna tofauti kati ya mweupe na mweusi katika vifo. Lakini wakifa weupe nakuambia ni kama wao wana haki zaidi. Hawastahili kufa. Mabomu ya London yaliyoua watu 54 hadi sasa yameonyesha hili. Viongozi mbalimbali wanatia saini vitabu vya maombolezo. Inatakiwa sasa kila asubuhi baadhi ya viongozi wakiamka asubuhi jambo la kwanza liwe ni kutia saini vitabu vya maombolezo kwa makumi ya watu wao waliohujumiwa maisha yao kwa Malaria, Kipindupindu, Ajali nakadhalika. Wasisahau pia kutia saini vitabu vya maombolezo kwa wananchi wa Iraq wanaouwa kila siku bila hatia.

Wednesday, July 13, 2005

Wanahabari ni muhimu kusoma hii

Hii tovuti ya John Pilger ni nzuri sana hasa kwa wana habari. Ipitie hapa halafu soma hii habari hapa

Unmfahamu George Galloway?

Huyu ni mwakilishi katika "House of Commons" Uingereza, anawakilisha eneo ambalo watu wake wengi walikufa katika milipuko iliyogharimu maisha ya waingereza wasiopungua 50 karibuni. Huyu bwana ameamua kusema ukweli. Anasema haya ni matokeo ya chuki ambayo imeongezeka dhidi ya Uingereza na Marekani kutokana na sera zao mbovu hasa huko Iraq, Afrighanistan, Mambo yanayotokea Guantanamo bay, yaliyotokea katika gereza la Abu Ghraib huko Iraq na mengineyo. Pamoja na kulaani hiki kitendo cha kulipuliwa waingereza kwa nguvu zote, bado anahoji mantiki ya kutoona wale wanaouwawa Iraq kila siku kama binadamu wengine. Anasema kuna watu wanaofikiri kwamba damu ya Wairaq waliouwawa Falujah wakati mji unateketezwa na wanajeshi wa ushirika ikiwemo Uingereza haina thamani kama waingereza waliouwa kwenye mashambulizi hayo. Tafadhali soma mawazo yake kama yalivyonukuliwa katika taarifa rasmi ya bunge (Hansard) Hapa

Tuesday, July 12, 2005

Kuna Demokrasia IMF na World Bank?

Kuna wataalam ambao wanahoji uhalali wa nchi kama Marekani kuwa na maamuzi makubwa katika vyombo vya fedha duniani yaani Benki ya Duniaa na Shirika la fedha ulimwenguni. Wanahoji pia uhalali wa nchi nyingine hasa changa kuwakilishwa na waziri wa fedha na gavana wa benki kuu tuu katika kutoa maamuzi makubwa ya nchi yao. Kwa wenye hoja kwamba nchi kubwa zina kura ya turufu kwa sababu ya mchango mkubwa, anatoa mfano wa Bill Gates kwamba yeye basi apatiwe kura kwa mfano laki moja kwa vile kipato chake kinaweza kuwa mara laki moja ya kipato cha mmarekani wa kawaida. Nisikumalizie uhondo, msome mwenyewe HAPA

Saturday, July 09, 2005

Mapadre na Familia

Soma habari hii ya mapadre wa Kanisa katoliki huko Marekani

Friday, July 08, 2005

Matatizo yameisha?

Mkutano wa wanyakua mali za waafrika umeisha. Nasikia sasa wamekubaliana kuongeza msaada kufikia Dola Bilioni Hamsini ($50). Kweli waafrika tuna matatizo mengi kweli. Baadhi yetu tulikuwa haturajii maajabu japo kuna watakaofikiri wamelamba dume. Hebu fikiria dola bilioni 50 kwa bara zima. Bara lina nchi 53 hivi zenye matatizo mengi na tofauti lakini nyingi ya nchi, matatizo yanafanana. Tukichukulia ukweli kwamba kuna nchi ambazo zina ahueni kama vile Mauritius, Nchi za Afrika ya kaskazini, Botswana, Afrika ya kusini, Namibia na nyingine chache, nchi nyingine ni hoi. Hata hizi si kwamba umasikini si wa kutisha, ni takwimu tuu ambazo zinaonyesha kwamba wana ahueni lakini kuna watu hoi ajabu na wengi. Sasa tukiziondoa hizo tuchukulie tunabaki na nchi kama 25 ambazo ni hoi zinazohitaji msaada huo. Ina maana kwamba kwa wastani kila nchi itapata Dola bilioni 2 hivi. Na haziji mara moja. Sidhani kama kuna maajabu yatakayotokea. Pili, huu utegemezi hautatutoa kwenye mtaro tuliopo.
Ninasikia huko Kenya watoto wamemkabidhi Balozi wa Uingereza sahihi kama 400,000 wakitaka nchi za kibepari zishughulikie matatizo ya watoto wa Afrika. Wanasema wanataka sahihi nyingine toka Uganda, Ethiopia na Tanzania ili zifike milioni moja. Watoto nao wameshakataa tamaa kwamba matatizo yao hayawezi kutatuliwa na nchi zao wanataka mabepari wayatatue. Sijuhi tunajengea watoto wetu kasumba gani. Kasumba ya kukosa imani na Serikali yao na kasumba ya utegemezi. Unafikiri hao watoto wanaweza kujua katika kukua kwao kwamba inawezekana kufanya chochote bila wazungu? Si ajabu watoto walivyowasilisha sahihi hizo kulikuwa na viongozi wa serikali, hata kama hawakuwepo huenda wamefurahishwa na jambo kama hilo, kwa sababu wanadhani mabepari wanaweza kuwasikiliza watoto na kupewa misaada ili yaingie tumboni mwao. Aibu hii!!!

Wednesday, July 06, 2005

Makala ya Misaada

Nimeandika mawazo yangu kuhusu misaada na mkutano wa G8. Unaweza kusoma hapa

Monday, July 04, 2005

Gadaffi aonya viongozi wenzake kuacha kuomba

Soma habari hii uone jinsi kiongozi wa Libya anavyowaonya viongozi wa Afrika kuacha kuomba kwa nchi tajiri. Nadhani waliozoea kutembeza bakuli wanamuona kama mwendawazimu fulani hivi.

Huenda Afrika ikagawanwa

Nahisi huo Mkutano wa G8 utakuja na mkakati wa kugawana maeneo Afrika. Kila mshirika atapewa vipande ambavyo ataambiwa avipe kipaumbele katika kutoa misaada. Kila nchi inaweza kukabidhiwa eneo Afrika kutokana na umahiri katika sekta fulani. Marekani nahisi itakuwa ni Equtorial Guinea, Cape Vedre, Chad sijuhi na ipi. Na nyingine zitachagua maeneo kutokana na uwezo wa kampuni zake kugecha rasilimali za Afrika. Ikitokea hivyo usishangae. Ndiyo Berlin Nyingine hiyo!!

Sunday, July 03, 2005

Angalia hii habari ya huyu Balozi wa Iraq

Habari hii hapa inaonyesha jinsi huyu balozi wa Iraq katika Umoja wa Mataifa alivyo mbinafsi. Analalamika kuuwa kwa binamu yake ambaye anadai hakuwa na hatia. Hivi ni maelfu mangapi ya wairaq wasio na hatia wanaouwa na jeshi la Marekani? Ameumwa sana na binamu yake anasahau kila mwiraq ambaye mtoto, mzazi au ndugu yeyote aliyeuwa ana machungu kama yake ila hawana pa kulalamikia kama yeye. Yeye kama mwakilishi ingebidi aongelee mfumo mzima wa utendaji wa jeshi la wavamizi wa marekani wanavyoua watu hovyo. Sasa kaona binamu yake ni binadamu zaidi kuliko wengine!

Saturday, July 02, 2005

Yanayotokea Malawi

Ukifuatilia mambo yanoyotokea nchi jirani ya Malawi tangu alipochaguliwa Bingu wa Muthalika utagundua mengi. Jambo la kwanza utakalogundua ni lile onyo alilowahi kutoa Hayati Mwalimu Nyerere: je unapotumia fedha lukuki kutaka urais utazilipaje? Kuna kiwanda cha kutengeneza pesa ikulu? Ndicho alichofanya Bakili Muluzi rais mstaafu. Alitafuta mamilioni ya Kwacha za Malawi kumnadi wa Muthalika. Baada ya kuchaguliwa akatakiwa aanze kuchota pesa kulipa madeni. Wacha utani, mchumi kakataa kata kata. Sasa wakaanza kumzushia visa wanataka sasa kumtosa kabisa. Wabunge wa UDF chama kilichompa urais kinataka sasa kulitumia bunge kumwadabisha. Malumbano yakawa makali mpaka Spika kapata kiharusi na sasa Marehemu.
Lingine ni kwamba huyu rais Muthalika ataandika historia. Nadhani atakuwa miongoni mwa watu wachache wenye uthubutu duniani. Uthubutu wa kukihama chama kilichompa madaraka na kuunda cha kwake. Si mchezo inahitaji roho ngumu hasa. Wamalawi wameshindwa cha kumfanyia kwa sababu katiba iko kimya iwapo rais ataamua kukihama chama. Nani angefikiria kwamba kuna mtu angethubutu kufanya hivyo? Huyu bwana atasaidia sasa nchi nyingi kuangalia katiba zao upya. Kuna jamaa wanaosema kwamba huyu bwana kafanya kitu ambacho hakijawahi kutokea nchi yoyote. Kama ni kweli basi yeye ni mwanzilishi. Kila kitu huwa na mwanzo kwani ni lazima ufanye mambo ambayo yameshafanyika tuu? Ni lazima kuwe na pa kuanzia. Nadhani atakumbukwa kwa hilo.
Mwisho, ni lazima ugundue kwamba unavyogombana na mtu na kusuluhishana ni wachache sana ambao husamehe kabisa. Muluzi na wa Muthalika walikuwa maadui wakubwa siku za nyuma. Inadaiwa kwamba ni Muluzi aliyemfanyia fitna wa Muthalika kuondolewa katika COMESA. Baadaye wakasuluhishana na Muluzi kumshika mkono kutaka wamalawi wamchague. Nadhani jamaa alikuwa akingojea pa kulipizia kisasi. Na sasa anafanyiza kweli!! Kuna somo tunaloweza kujifunza?

KITABU CHA WAGENI