Friday, July 08, 2005

Matatizo yameisha?

Mkutano wa wanyakua mali za waafrika umeisha. Nasikia sasa wamekubaliana kuongeza msaada kufikia Dola Bilioni Hamsini ($50). Kweli waafrika tuna matatizo mengi kweli. Baadhi yetu tulikuwa haturajii maajabu japo kuna watakaofikiri wamelamba dume. Hebu fikiria dola bilioni 50 kwa bara zima. Bara lina nchi 53 hivi zenye matatizo mengi na tofauti lakini nyingi ya nchi, matatizo yanafanana. Tukichukulia ukweli kwamba kuna nchi ambazo zina ahueni kama vile Mauritius, Nchi za Afrika ya kaskazini, Botswana, Afrika ya kusini, Namibia na nyingine chache, nchi nyingine ni hoi. Hata hizi si kwamba umasikini si wa kutisha, ni takwimu tuu ambazo zinaonyesha kwamba wana ahueni lakini kuna watu hoi ajabu na wengi. Sasa tukiziondoa hizo tuchukulie tunabaki na nchi kama 25 ambazo ni hoi zinazohitaji msaada huo. Ina maana kwamba kwa wastani kila nchi itapata Dola bilioni 2 hivi. Na haziji mara moja. Sidhani kama kuna maajabu yatakayotokea. Pili, huu utegemezi hautatutoa kwenye mtaro tuliopo.
Ninasikia huko Kenya watoto wamemkabidhi Balozi wa Uingereza sahihi kama 400,000 wakitaka nchi za kibepari zishughulikie matatizo ya watoto wa Afrika. Wanasema wanataka sahihi nyingine toka Uganda, Ethiopia na Tanzania ili zifike milioni moja. Watoto nao wameshakataa tamaa kwamba matatizo yao hayawezi kutatuliwa na nchi zao wanataka mabepari wayatatue. Sijuhi tunajengea watoto wetu kasumba gani. Kasumba ya kukosa imani na Serikali yao na kasumba ya utegemezi. Unafikiri hao watoto wanaweza kujua katika kukua kwao kwamba inawezekana kufanya chochote bila wazungu? Si ajabu watoto walivyowasilisha sahihi hizo kulikuwa na viongozi wa serikali, hata kama hawakuwepo huenda wamefurahishwa na jambo kama hilo, kwa sababu wanadhani mabepari wanaweza kuwasikiliza watoto na kupewa misaada ili yaingie tumboni mwao. Aibu hii!!!

KITABU CHA WAGENI