Saturday, July 02, 2005

Yanayotokea Malawi

Ukifuatilia mambo yanoyotokea nchi jirani ya Malawi tangu alipochaguliwa Bingu wa Muthalika utagundua mengi. Jambo la kwanza utakalogundua ni lile onyo alilowahi kutoa Hayati Mwalimu Nyerere: je unapotumia fedha lukuki kutaka urais utazilipaje? Kuna kiwanda cha kutengeneza pesa ikulu? Ndicho alichofanya Bakili Muluzi rais mstaafu. Alitafuta mamilioni ya Kwacha za Malawi kumnadi wa Muthalika. Baada ya kuchaguliwa akatakiwa aanze kuchota pesa kulipa madeni. Wacha utani, mchumi kakataa kata kata. Sasa wakaanza kumzushia visa wanataka sasa kumtosa kabisa. Wabunge wa UDF chama kilichompa urais kinataka sasa kulitumia bunge kumwadabisha. Malumbano yakawa makali mpaka Spika kapata kiharusi na sasa Marehemu.
Lingine ni kwamba huyu rais Muthalika ataandika historia. Nadhani atakuwa miongoni mwa watu wachache wenye uthubutu duniani. Uthubutu wa kukihama chama kilichompa madaraka na kuunda cha kwake. Si mchezo inahitaji roho ngumu hasa. Wamalawi wameshindwa cha kumfanyia kwa sababu katiba iko kimya iwapo rais ataamua kukihama chama. Nani angefikiria kwamba kuna mtu angethubutu kufanya hivyo? Huyu bwana atasaidia sasa nchi nyingi kuangalia katiba zao upya. Kuna jamaa wanaosema kwamba huyu bwana kafanya kitu ambacho hakijawahi kutokea nchi yoyote. Kama ni kweli basi yeye ni mwanzilishi. Kila kitu huwa na mwanzo kwani ni lazima ufanye mambo ambayo yameshafanyika tuu? Ni lazima kuwe na pa kuanzia. Nadhani atakumbukwa kwa hilo.
Mwisho, ni lazima ugundue kwamba unavyogombana na mtu na kusuluhishana ni wachache sana ambao husamehe kabisa. Muluzi na wa Muthalika walikuwa maadui wakubwa siku za nyuma. Inadaiwa kwamba ni Muluzi aliyemfanyia fitna wa Muthalika kuondolewa katika COMESA. Baadaye wakasuluhishana na Muluzi kumshika mkono kutaka wamalawi wamchague. Nadhani jamaa alikuwa akingojea pa kulipizia kisasi. Na sasa anafanyiza kweli!! Kuna somo tunaloweza kujifunza?

1Comments:

At 2:26 PM, Anonymous Mary said...

Hii ni taarifa ya maana, yapasa kila mtu kuijua

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI