Saturday, June 25, 2005

Kitabu cha kusoma

Jamani kuna hiki kitabu nilichokisoma mara mbili kinaitwa Secret Terrorists kilichoandikwa na Bill Hughes. Jamaa huyu amendika mengi sana yote yakihusu jinsi ambavyo Kanisa Katoliki kwa muda mrefu limekuwa likihujumu taifa la Marekani na Dunia kwa ujumla. Baadhi ya madai haya ni Pamoja na Njama za kumuua rais Andrew Jackson aliyechaguliwa kuwa rais mwaka 1828 jaribio lililoshindikana; kuuwa kwa rais William Hendry Harrison aliyechaguliwa kuwa rais mwaka 1841 rais Zachary Taylor aliyechaguliwa mwaka 1848, jaribio lingine la kumuua Rais James Buchanan kwa sumu lililoshindikana; kuuwa rais Abraham Lincoln na John F.Kennedy. Chanzo cha mauaji na majaribio haya kwa mujibu wa mwandishi ni kutokana na marais hawa kupingana na matakwa ya wanaojulikana kama Jesuits chini ya Kanisa Katoliki.

Madai mengine ya nguvu ni pamoja na kuzamishwa kwa meli ya TITANIC mwaka 1912 kwa lengo la kuwaua matajiri watatu maarufu duniani wakati huo Benjamin Guggenheim, Isador Strauss na John Jacob Astro walioonekana tishio katika kuzuia kuanzishwa benki kuu ya Marekani inayomilikiwa na matajiri wachache wa Jesuits.

Vita ya kwanza na pili ya Dunia pia anasema ilianzishwa kwa mkono wa kanisa hilo. Hitler na Mussolini inasemekana walikuwa wakiungwa mkono na Kanisa Katoliki. Matokeo mengine yanayozungumziwa kwenye kitabu hicho ni pamoja na maovu yaliyofanywa na Slobodan Milosevic katika kuwamaliza Wakristo wa Madhehebu ya Kiorthodox huko Serbia miaka ya 1990. Mwandishi anadai muuji si Milosevic bali ni Papa na Kanisa Katoliki hata kumshitaki bwana Milosevic ni uonevu tuu.

Jamaa anaendelea kutupasha kwamba matokeo ya Septemba 11 ni mtiririko huo huo hakuna cha Osama wala nini kama hakukuwa na Osama mwaka huo wa 2001 basi angeundwa Osama mwingine ili kulinda maovu ya hao majamaa.

Jamani yote tisa lililoniacha hoi ni hili dai kwamba: Vatican ilianzisha Uislamu kwa lengo la kuwaangamiza wakristo na wayahudi, kulinda wakatoliki na kuiteka Jerusalemu ili waikabidhi kwa Papa. Katika miaka michache ya mwanzo ya uislamu, waislamu walifanya hivyo lakini ilipofikia hatua ya majenerali wa kiislamu kuisalimisha Jerusalemu kwa papa waligundua kwamba walikuwa na uwezo wakakataa kuisalimisha. Hata vita ya ugaidi inayoendelea leo ni moja ya njia za kuwalipiza waislamu kwa kukataa wakati huo kuikabidhi Jerusalemu kwa Papa. Kwa hiyo vita ya mashariki ya kati itaendelea, watakufa watu kwa maelfu hadi hapo mpatanishi atakapotafutwa na mpatanishi huyo atakuwa papa na kwa vile vyombo vya habari vilivyothibiwa vitashawishi ulimwengu kwamba anayeweza kutatua tatizo la mashariki ya kati ni papa pekee, atafanya hivyo na ataiteka Jerusalem. Hapo misheni itakuwa imefanikiwa kwa sababu lengo limekuwa wakati wote huu ni kuitwaa Jerusalemu.

Nimedonoa tuu kijitabu hiki nakushauri ukisome. Kisome kwa makini nahisi kimeandikwa na msabato. Kwa wale wanaowaelewa wasabato haitakuwa ngumu kuelewa kwa nini ninasema hivyo. Binafsi nina maswali lukuki ya kumuuliza huyu mwandisi najaribu kuwasiliana naye ili anijibu maswali yangu. Nitawaeleza maendeleo ya mjadala wangu na huyu bwana. Mwenye habari ya ziada juu ya madai haya yaweke adharani watu wayaone na wayajadili.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI