Monday, June 20, 2005

Jamani nani anatoa mgao wa saluti?

Nilitaka kukaa kimya bila kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya wabunge kutaka wapigiwe saluti. Mimi nauliza ni nani mtoa mgao wa saluti? Ni waziri? ni nani? Kwa nini asiwagawie tuu. Nadhani wabunge wamegundua kitu kwenye saluti. Ni lazima wakishapigiwa saluti wananchi wa majimbo yao watapata hali nzuri ya maisha, ni lazima uzalishaji wa chakula utaongezeka, ni lazima masoko ya bidhaa zao yatapatikana, ni lazima umasikini Tanzania utapungua kwa kasi ya ajabu. Nina mategemeo kwamba wakipewa mgao wa saluti malengo yanayoitwa ya milenia yanaweza yafikiwe kabla ya muda wake tukaweka historia. Sidhani kama mtu anaweza kudai saluti kama haimuongezei mwananchi hali nzuri ya maisha. Naomba mtoa mgao afikirie hili. Baada ya kufikiria kuwapa wabunge, na ili kasi ya maendeleo iongezeke kwa kishindo, basi na atoe mgao kwa madiwani wa kata zote nao wapewe saluti zao hawa wako karibu na wananchi zaidi kuliko wabunge. Baada ya hapo viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji wapewe mgao wao, asisahau balozi wa nyumba kumikumi. Nadhani hawa waote wakipewa mgao wa saluti basi mwaka kesho mwezi kama huu tutakuwa tumefikisha malengo ya milenia.
Ili kasi ya maendeleo iongezeke kwa kasi ya ajabu na Tanzania iwe nchi ya dunia ya kwanza kwa kwa kipindi kifupi, viongozi wote walio karibu na wananchi wakabidhiwe saluti zao. Viongozi wa dini wapewe. Dini zote. Maaskofu wote. Mapadre wote. Baba Paroko wote. Viongozi wote wa vigango. Wachungaji wote. Mashemasi wote na waingilisti wapewe mgao wao. Masheikh wote akianzia mkuu, wa mikoa wa wilaya na maimamu wote wakabidhiwe mgao wao. Viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wapewe pia. Nadhani tukiongeza kasi ya mgao ndivyo na kasi ya maendeleo itakavyoongezeka. Tusibanie saluti la sivyo tutabaki kuwa masikini mpaka kiama.

2Comments:

At 10:51 PM, Anonymous Anonymous said...

Nisipocheka basi lazima nitakuwa na tatizo la kwenye kemikali zinazofanya binadamu acheke. Lakini pia nisipojua kwa undani unachosema, itakuwa nimepoteza muda bure kusoma habari hii.

 
At 12:20 PM, Blogger Indya Nkya said...

Usione unapoteza muda. Soma jaribu kuelewa. Nadhani umeelewa. Ni nini kinaleta chakula mezani? Saluti? Kuna mambo mangapi ambayo wabunge wanaweza kuyaongea kwa nchi yenye matatizo kama Tanzania? kudai saluti ni nini? Ni lazima wamegundua saluti zina umuhimu wake katika kuharakisha maendeleo.

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI