Tuesday, June 28, 2005

Mambo ya Yakobo

Sikutaka kuandika chochote kuhusu sakata la Yakobo Zuma, Makamu wa zamani wa Rais wa Afrika ya Kusini kutimuliwa kwa madai ya rushwa, lakini wapi, wachokozi wametaka niseme lolote. Basi ninasema. Miezi mitatu iliyopita nilijikuta nabishana na jamaa wawili toka Zambia. Hawa jamaa nilisafiri nao kwa masaa kama 18 hivi, tuliongea mambo mengi likiwepo sakata la Rushwa lililokuwa likimkabili Yakobo. Jamaa mmoja kati ya hawa anadai ni mzoefu wa mambo ya Afrika ya Kusini akaniambia; unajua sakata la Yakobo na rushwa si la kweli? Ni uzushi mtupu, ni mambo ya siasa tuu. Nikamuuliza kivipi? Akaniambia ni mambo ya ukabila, Yakobo ni Mzulu, na watu wa kabila la Waxhosa ambalo wanatokea pia Mandela na Mbeki hawataki mzulu awe rais kabisa kwa hivyo wameamua kumzushia kashfa ili wamtose kwa kuwa umakamu wa rais ungempa nafasi nzuri ya kuwa rais. Akaendelea, hata wazungu hawataki wazulu kwa sababu wazulu si mchezo, ni watu wa shari na walipiza kisasi. Kwa hivyo Yakobo amekumbana na janga kama hilo. Uzulu umemponza. Nikamuuliza huyu jamaa, sasa kwa nini wamwache au wampe vyeo mpaka umakamu wa rais? Jamaa haishiwi na hoja. Akaniweka chini na kuniambia: unajua walimweka pale kukimaliza chama cha Inkatha Freedom cha Mongusuthu Buthelezi ambacho kilikuwa na nguvu kubwa miongoni mwa wazulu na sasa si unaona Inkatha hoi? Kamaliza kazi na sasa anatoswa.

Kwa kweli kama si mambo ya aibu waliyokumbwa nayo kina Chiluba basi huyu bwana angeniaminisha kwa sababu mimi kuna jambo moja nashindwa na nitashindwa kuelewa mpaka kesho. Hivi kwa nini kiongozi wa ngazi za juu kama rais, makamu wa rais au waziri mkuu wakumbwe na kashfa za kijinga za wizi au Rushwa? Ukiona kiongozi anakumbwa na kashfa kama hii basi ni mjinga. Hawa watu wanatunzwa kwa kodi za wananchi wakiwa madarakani, wakistaafu wanaendelea kutunzwa mpaka wafe. Si wao tuu mpaka na wake zao hata kama unao wawili watakutunzia mpaka wafe. Sasa kwa nini unaiba tena? Mimi narudia tena, binadamu ni kiumbe wa ajabu kuliko kingine chochote.

Sasa haya ya Yakobo tutangoja tuone kama kweli ni safi au ni mla rushwa tuu baada ya yeye mwenyewe kujitetetea mbele ya mahakama. Hata yeye mwenyewe amesema ni mambo ya siasa na si mla rushwa, tuongoje tuone kama tutamweka kwenye kundi la viongozi wajinga wa Afrika au la. Kutakuwa na kasheshe, huko kwao Durban washabiki wake wamekuja juu vibaya sana, kila waziri mkuu wa jimbo la Kwazulu Natal anapotaka kuwahutubia wananchi, washabiki wa Yakobo wanavuruga mkutano. Hawaambiwi chochote wakaelewa.

2Comments:

At 2:12 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Nimeambiwa na jamaa mmoja maelezoi kama yako kabisa. Afrika Kusini kuna rushwa sana katika viambaza vya utawala, kwanini Mbeki kamvalia njuga Zuma tu?

 
At 12:13 PM, Blogger Indya Nkya said...

Inaelekea asingekuwa mzulu asingevaliwa njuga ingezimwa kimya kimya

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI