Saturday, December 17, 2005

Igizo limeisha, tungoje miaka mingine mitano

Mchezo wa kuigiza umekwisha. Miaka mingine mitano wananchi watalishwa tena maneno, pilau, khanga, sukari watauza tena kura zao. Mchezo unaendelea. Lakini mchezo huu utaendelea hadi lini? Na watanzania tulivyo hatutawauliza wale walioshinda chochote hata kama hawatatimiza moja kati ya walioahidi. Lakini hata hivyo ni wangapi tunakumbuka hata ahadi zenyewe? Pilau na khanga na fulana zinatosha. Jamaa mmoja kaniacha hoi sana. Ameniambia jinsi ambavyo bado kuna kibarua kigumu mbele yetu. Alishuhudia watu wakibishana baada ya kampeni. Hawakubishana chochote kuhusu yaliyozungumzwa kwenye mkutano wa kampeni. Ubishi ulikuwa juu ya vifaa na magari ya vyama vyao. Mmoja akiwa anasema umeona spika za chama chetu? Ni nzito bwana si mchezo. Mwingine akamwambia acha utani, uliona gari walilokuwa wakitumia wagombea wa chama changu walipokuja hapa? Kazi ipo. Kwa kweli kama tunataka mabadiliko inabidi tusilale usingizi. Tupambane kweli.


KITABU CHA WAGENI