Tuesday, May 03, 2005

Ni kuongoza tuu?

Nimekuwa najiuliza swali hili kila mara. Hivi watu wanavyogombea uongozi nia yao huwa ni kuongoza tuu? Nilianza kujiuliza swali hili zamani sana. Sielekei sana kugundua sababu hasa ya hata mtu kwenda "kwa Babu" kutafuta uongozi. Hivi kuongoza tuu watu unakutolea macho hivyo? Nadhani sababu ni nyingi mno. Kuongoza ni kajisehemu kadogo sana ka sababu hizo. Sidhani kama utaenda kwa babu ili tuu uongoze watu. Watu wanapenda ujiko bwana. Kutambulika. Kuitwa mheshimiwa badala ya ndugu fulani. Kuna wakati bunge lilipoteza muda wa wapiga kura wao mwingi wakijadili kwamba sasa waitwe waheshimiwa na si ndugu au bwana au bi au bibi. Ni lazima watofautishwe na wengine. Sijuhi ni mpiga kura gani aliwatuma kwenda kujadili hayo mambo. Uheshimiwa unakuja tuu hata bila kuutungia kanuni. Timiza wajibu wako, fanya kazi kwa bidii. Toa mchango kwa jamii yako (si mchango wa harusi) mchango wa maendeleo- simanishi pesa hapa. Mawazo, kukusanya rasilimali watu zilizopo katika jamii, tambua uwezo wao, weka mawazo yao pamoja, buni mkakati wa maendeleo pamoja. Baada ya hapo utaona utaitwa mheshimiwa sana. Hutahitaji kwenda kujadili bungeni utambuliweje. Uchaguzi wa urais ndio huo. Watu nasikia wanachafuana vibaya sana. Wanapigana vikumbo. Wanapigania nafasi moja ambayo itakuja tena baada ya miaka kumi. Wanataka kuongoza watanzania. Je ni kuongoza tuu? Ni maslahi binafsi? ni kuitwa mheshimiwa, mtukufu mpendwa wetu rais........ Ni ving'ora vya kutishia wananchi wako na kusafirishwa kwa mwendo wa kasi kama vile unatorishwa au? Lazima tuwaulize hawa jamaa swali hili: Kwa nini unataka kuwa rais? Ukishapata jibu muulize kwa nini utumie sana nguvu, uchafu, matambiko na mambo mengine ya ajabu? Kuna la zaidi si kuongoza tuu.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI