Tuesday, May 03, 2005

Utamaduni wa kuambiana Ukweli

Ukifuatilia matatizo yanayotokea Togo sasa hivi utagundua kwamba yamechangiwa na utamaduni wa waafrika wa kutotaka kuambiana ukweli. Wakati Eyadema mzee alipofariki Febuari mwaka huu na Mwanaye Faure kumrithi kusivyo halali, Jumuiya ya ECOWAS iliingilia kati kuataka kutatua mgogoro huo lakini ikautatua kwa kutoambiana ukweli. Baadhi ya watu waliwasifu sana ECOWAS kwa kumlazimisha Faure aondoke madarakani na baadhi wakaanza kuilaumu sana SADC kwamba imeshindwa kumlazimisha Mugabe aondoke madarakani. Hawa niliwaambia kwamba hakuna suluhisho la kudumu kwa Togo kwa kuwa Faure atakuja madarakani kwa kile kinachoitwa "uchaguzi wa kidemokrasia". Walichosahau ni kwamba Watogo wamechoshwa na jina la Eyadema kwa njia ya uchaguzi au kijeshi au vyovyote vile. Baba katawala kwa zaidi ya miongo mitatu, mwanaye naye sasa atatawala kwa miaka kadhaa kwani bado ni kijana-ana miaka 39 tuu. Baadaye nikaangalia kipindi cha "Hard Talk" cha BBC kilichoendeshwa na Lyce Docet akimhoji katibu mtendaji wa ECOWAS, kati ya mambo mwanadada huyu aliyombana nayo katibu huyu ni tetesi kwamba baada ya mazungumzo ya kumtaka Faure aondoke madarakani na yeye kuonekana kukataa, ECOWAS walimhakikishia kwamba angerudi madarakani kwa njia ya uchaguzi. Ndipo bwana huyu akakubali kuachia madaraka ya kupora. Kama tetesi hizi ni kweli basi ECOWAS inawajibika pia kwa matatizo yanayotokea Togo na yatakayozidi kutokea kwa kutosema ukweli kwamba watu wamelichoka jina la Eyadema. Hili ndio tatizo la kutoambiana ukweli. Tujenge utamaduni wa kuambiana ukweli hasa kwenye siasa.


0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI