Wednesday, May 11, 2005

Uwezo wa kuhoji

Watu wanapokuwa wamebanwa kisawasawa, wanakuwa wanafikiria tuu namna ya kupata chakula cha leo. Si kesho wala keshokutwa. Si Elimu wala chochote kingine. Ni chakula kwanza. Utafikiriaje chochote wakati njaa imefanya makao makuu kwenye tumbo lako? Hii ndiyo hali halisi inayowakabili watanzania wengi na hasa vijana. Hali ya ajira ni mbaya sana. Vijijini hakukaliki. Wakati mwingine tunawalaumu watanzania kwamba ni wavivu. Kama ukitaka kujua si wavivu kiasi cha kutisha, safiri kuanzia Tunduma mpaka Dar-es-Salaam, ona mazao yalivyopangwa barabarani kwa bei ya kutisha. Nina maana bei ndogo kabisa. Nenda Shoprite (kama Si Shopwrong) uone vitunguu na nyanya toka "bondeni" ambavyo vimekuzwa kimaajabu. Kwa ufupi ni kwamba mazingira ya vijijini hayavutii kukaa. Mimi nina imani kubwa sana hakuna kijana atakayekubali kuja kuhangaika siku nzima mjini akiuza shati moja kama angeweza kulima nyanya zake na zikamrudishia fedha zake. Kijana kama huyu anayefikiria chakula cha leo hawezi kuhoji mgombea anayemwambia atampatia ajira. Anachoangalia ni lini tarehe 30 oktoba itafika akapige kura ili mgombea apite na apate ajira. Kwamba itapatikanaje hataki kuhoji, hata nguvu za kuhoji hana. Angekuwa na uwezo angesogeza kalenda mbele ili Oktoba ifike mapema apate ajira yake. Kwake hajuhi hata kama mgombea ana mpango kabambe wa kuongeza ajira itamchukua muda mrefu kabla huo mpango kabambe haujafanikiwa. Kama ni kuanzisha viwanda itabidi vijengwe (Sitaki kuingia ndani sana hapa, naanzia tuu kwenye ujenzi), vikamilike vianze uzalishaji. Vyovyote vile ni lazima kutakuwa na maandalizi yatakayochukua muda mpaka ajira izalishwe. Ukweli huu ndio hao vijana watatakiwa waujue.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI