Saturday, October 29, 2005

Uganda imeendelea sana, haiitaji msaada wa IMF

Kuna habari inayoifagilia kweli nchi ya Uganda ilivyopiga hatua ya kimaendeleo. Sijuhi. Kama vigezo walivyotumia ni sahihi basi Uganda iko mbali. Lakini kama ni suala la kucheza na takwimu tuu, basi kila nchi inaweza kuonekana imeendelea au haijaendelea. Naziogopa sana takwimu japo nacheza nazo kila ukicha. Kwa upande mwingine licha ya maendeleo haya, bajeti ya uganda inafadhiliwa kwa asilimia kama 50 hivi na wahisani wa nje. Innocent tuambie. Mtaani Uganda mambo yakoje? Soma habari hiyo hapa

Barua kwa rais mtarajiwa

Kuna Wazalendo wawili waliomwandikia rais mtarajiwa barua wakimtafadhalisha kwamba serikali ijayo ifanye mambo ya muhimu kwanza. Barua hiyo imetoka kwenye gazeti la Rai la Alhamis tarehe 27/10/2005. Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa. Ukiwa na la kuwauliza waandikie: sakitomalya2001@yahoo.co.uk

Thursday, October 27, 2005

Ethan akiri ugwiji wa Ndesanjo

Ethan Amekubali kwamba Ndesanjo Si mchezo jinsi alivyoweza kuhabarisha wasomaji wake kilichokuwa kinaendelea katika mkutano wa Pop Tech huko Camden. Kilichomuacha hoi ni jinsi Macha alivyoweza kuandika karibu kila kitu kilichokuwa kikiendelea tena akitafsiri kwa kiswahili. Lazima na mimi nikupongeze kwa hili ndugu yangu. Ongeza bidii. Lisha jamii habari Mangi. Ukifungua blogu ya Ethan utakumbana na hiyo habari. Tumpe Ndesanjo hongera zake kwa hili. Ukibonyeza HAPA utasoma kwa undani alichosema Ethan

Wednesday, October 26, 2005

Sawa si sawasawa tena

Fide aliuliza binadamu wote ni sawasawa? Macha sasa nadhani huitaji mjadala tena. Kuna huyu mtu anayeitwa Magufuli -Waziri wa Ujenzi. Anasifika sana kwamba anachapa kazi. Lakini mgongoni mwa huo uchapa kazi ana mambo ya kusikitisha mno. Soma hapa uone moja ya mambo yake mengi ya ajabu.

Monday, October 24, 2005

Mijadala, mijadala na mijadala

Leo nilikuwa kwenye mjadala mmoja kuhusu mambo yanavyokwenda hapa Afrika ya Kusini. Waongeaji katika mjadala ule walikuwa rais wa zamani F.W. De Klerk na mtu anayeitwa Tokyo Sexwale. Huyu Sexwale ni mweusi ambaye alikuwa kati ya wapambanaji waliofungwa miaka mingi huko Robin Island. Lakini baada ya miaka 11 tuu ya utawala wa weusi amekuwa ni tajiri mkubwa sana. Mjadala ule ulikuwa wa kufurahisha. De Klerk anasema kwamba weupe wanaogopa sana hiki kinachoitwa Black Empowerment kwa sababu hatma ya weupe haijulikani na sasa baadhi wameanza kuwapeleka watoto wao nje ya nchi wakihofia kitakachotokea kwani huenda wakatengwa kiajira na mambo mengine. Anadai pia kwamba umasikini umeongezeka licha ya uchumi kukua. Kwa mfano anasema pengo kati ya walio nacho na wasionacho limekuwa sasa zaidi ilivyokuwa kabla ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi. Idadi ya weusi wasio na ajira imeongezeka kuliko kabla ya utawala wa kibaguzi. Madai yake kwa kweli ni ya msingi hasa ya ongezeko la umasikini na kukua kwa pengo la matajiri na masikini. Hoja yake nyingine ni kwamba kuwawezesha weupe haina maana kuwapa kazi za juu au fedha za biashara hata kama hawana uwezo huo. Uwezeshaji mkubwa ni kuwaelimisha ili waweze kushindana katika soko. Hili nalo halina ubishi.
Sexwale akasema kwamba licha ya kelele zote zinazopigwa, bado weusi hawajapata chochote cha kutisha. Ametoa mfano kwamba Katika soko la hisa la Johanesburg, weusi wanamiliki asilimia 1.8 tuu ya trilioni moja ya hisa zote. Hii ni baada ya miaka 11 ya utawala mpya. Akasema pia kwamba maajabu yasitarajiwe kwa kipindi kifupi kama hiki. Kwa maneno mengine watu weusi pia wasitarajie kila kitu kitamalizika kwa miaka 11 tuu. Lakini hakutuambia yeye amewezaje kuwa tajiri hivyo kwa miaka 11 tuu.
Niliwahi kusema huko nyuma kwamba Afrika ya Kusini imeshazalisha tabaka jingine la matajiri wachache weusi ambao wanapewa mitaji ya biashara na vyeo vikubwa badala ya kuimarisha elimu kwa weusi kwa ngazi zote kwanza. Leo hii kuna mamilioni ya watoto weusi hawana madawati wala viti vya kukalia mashuleni. Badala ya kuanza kuimarisha kizazi kijacho ili kiweze kushindana na hao weupe miaka ijayo wanazalisha mabilionea wachache halafu wanaacha lundo la weusi wakiangaika pasipo kazi wala elimu nzuri. Ukisikiliza mijadala yao utagundua kazi bado ipo.

Sunday, October 23, 2005

Dawa za ARVs husababisha magonjwa ya moyo

Kuna habari hii hapa inayosema kwamba dawa za kurefusha maisha husababisha magonjwa ya moyo. Tafadhali isome. wakati fulani kwenye blogu yangu ya kiingereza niliandika kuhusu hili jambo nikijenga hoja kwamba wale walioshtaki kampuni iliyokuwa ikitengeneza dawa za kutuliza maumivu ziitwazo VIOXX na baada ya kuzitumia mgonjwa magonjwa ya moyo hawakuwa wajinga na inawezekana kabisa kwamba kampuni hizi zinazotengeneza ARVs baadaye zikashtakiwa. Jamaa mmoja kanijia juu kishenzi. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba dawa hizi zina madahara makubwa sana katika mwili.

Thursday, October 20, 2005

KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI

Nimekutana na maoni ya mzalendo mmoja kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili nikaona nishirikiane nanyi kupata anachosema: maoni yake nayaweka hapa chini:
KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI
Mzee Nimejifunza yafuatayo na siyo vibaya tukichangia:
(1) Kule Mbeya, Bukoba, Moshi, Iringa na sehemu nyingi zenye baridi watu wanakunywa zaidi CHAI ya kahawa. Wakati sehemu za joto joto kama Dar hawana chaguo maalumu, hata CHAI ya siturungi, milo, cocoa,zote zinanywewa bila mpangilio wowote.
(2) Yule NYERERE wa Msumbiji aliyekuwa akiitwa SamoraMasheli alikufa kwa ajali ya ndege na wala siyo gari.Na NYERERE wa Libya, Gadafi huenda akawa ndiyekiongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu. Somali wao hawana NYERERE bado, hii ni kwa ajili yamachafuko ya kivita.
(3) Kila nchi duniani hutumia lugha ya KISWAHILI kuunganisha jamii zao za makabila mbalimbali na kufundisha katika ngazi na nyanja zote za elimu. Mfano, Uganda, Malawi, Zambia, n.k., wao hutumia KISWAHILI cha Kiingereza. Gabon, Congo, Senegal, n.k.wao hutumia KISWAHILI cha Kifaransa; England, Wales,Marekani na Scotland hutumia KISWAHILI cha Kiingereza;Misri, Libya, Tunisia, n.k. wao ni KISWAHILI chaKiarabu; Uchina nasikia ni KISWAHILI kinachoitwa Mandarin; Arjentina, Kolombia, Chile, n.k. niKISWAHILI cha Kiispania, Urusi ni Kirusi, Ureno naBrazili na Angola ni Kireno, n.k. n.k.?
(4) Nchi yetu Tanzania ambayo KISWAHILI chake ni Kiswahili, ndiyo nchi pekee duniani ambayo imetumia KISWAHILI kuunganisha watu wake wa makabila mbalimbali halafu maajabu imekataa kutumia KISWAHILI hicho hichokatika kutoa na kupokea elimu mashuleni na vyuoni mwake !!!!!!!!!!!!. Hii inamaanisha kuwa kinachofundishwa mashuleni kwetu siyo elimu bali mahudhurio ya semina ndefu ndefu tulizozibatiza majina; Form IV, IV na madigirii.Nadhani vyeti vyake sahihi vingeitwa VYETI VYAMAHUDHURIO YA SEMINA YA FORM IV, n.k. na siyo vyeti vya ELIMU. Neno elimu ni pana na kubwa. Hivyo lisitumike pasipostahili. Vinginevyo ni sawa na kudai kuendesha kilimo cha minazi wakati shamba zima umepandikiza makuti mabichi!! Na misingi ya kukataa kutoa elimu kwa KISWAHILI ndiyo chanzo cha umaskikini wetu pamoja na kuwa matajiri wenye raslimali lukuki:watu takribani milioni 40, ardhi yote yenye rutuba,maji hadi kiama - yawe chumvi au baridi, hali ya hewa murua - hakuna vimbunga-matetemeko ya ardhi-baridi na joto zinazoua, madini kila aina nchi nzima, mbuga za wanyama duniani hakuna na lugha ya KISWAHILI iliyo pevu. Nchi zote duniani zinapotoa elimu kwa KISWAHILI chake,siyo wapumbavu, hivyo na sisi tuanze leo. Anayedai lugha haijakuwa bado, mwambie akupangia lugha ya kwanza hadi ya mwisho kama ataweza, hawezi, kwani hakuna kitu kama lugha changa. Anayesema tutafsiri kwanza vitabu kutoka lugha za kigeni - muulize mbona tunatumia maneno kama motokaa, oksijeni, pasipoti,kompyuta, redio na wenzetu nao wanatumia maneno yetu kama panga, shamba, safari, kimeharibika nini?. Anayedai hatutatambulika duniani - kwanza, waulize duniani kuna nchi ngapi zisizotumia hiyo lugha ya kigeni tunayoikumbatia - na wanatambulika zaidi yetu??pili wafahamishe kiswahili kinasambaa kama moto wa mbugani. Wasikilize Wakongo, Waburundi na Rwanda,Wakenya, Wamsumbiji, n.k. wanavyokiongea. Tatu waombe wasikilize redio Ujerumani, Peking, Sauti ya Amerika,BBC, n.k. Mwisho waelimishe kuwa wanapodai kuwa lugha haijakuwa, hatutatambulika, n.k huwa wanamaanisha,tena bila kujitambua wala aibu, kuwa wao ni wanyonge,dhaifu, wasiojiamini, wasioweza kujiendesha wenyewe,watumwa - haswa haswa huko vichwani mwao na wasiotakakuelimika.
Kwaheri,
Kiswahili chema,

Wednesday, October 19, 2005

Paper ya Prof. Othman

Profesa Haroub Othman wa Chuo Kikuu cha DSM alikuwa msemaji Mkuu kwenye Mhadhara wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ulioandaliwa na chuo hiki hapa tarehe 14/10/2005. Mada aliyotoa ilikuwa: Nyerere an Intellectual in Power. Isome kwa kubonyeza hapa

Tuesday, October 18, 2005

Misaada ya Nje jamani!!

Katika soma soma yangu nimekutana na sentensi ifuatayo: "At one point in Tanzania, the total for government wages and salaries (which are taxed) was $100 million, while the salary bill for technical assistants supplied under aid programs (and not taxed) was $200 million". Yaani mishahara inayotokana na misaada ambayo hailipiwi kodi kwa wakati huo ilikuwa mara mbili ya ile serikali. Tunapoteza kodi kiasi gani?

Monday, October 17, 2005

Makala ya kumkukumbuka Mwalimu

Niliandika makala kumkumbuka Mwalimu J. K. Nyerere ambayo ilitoka kwenye gazeti la Rai la tarehe 13/10/2005. Nakuwekea hapa uisome

Parched Earth

Padre Karugendo amemwandikia barua ya pongezi Mwandishi wa Kitabu cha Parched Earth mama Elieshi Lema. Ukisoma barua hiyo unaweza kupata mawili matatu yaliyomo kwenye kitabu hicho ambacho ni kizuri na muhimu mno. Unaweza kuisoma hapa. Kumbuka makala zake nyingine zipo kwenye kona yake ndani ya Blogu hii

Maajabu haya!!

Jamaa wa Kanisa la Ephata wameamua kwenda Israel kuombea uchaguzi mkuu na pia mahusiano mazuri kati ya Israel na Tanzania. Wakati huo huo Huyo kiongozi wao anawambia watanzania wengine waombee uchaguzi. Hivi, kwa nini wasingeombea wote nyumbani mpaka waende Israel? Kama anaona Israel ni mahali patakatifu ambapo sala zao zitakubalika zaidi, kwa nini sasa awaambie watanzania wengine wanaosalia nje ya Israel waendelee kuomba? Ndesanjo atalieleza vizuri hili. Halafu anataka uhusiano na Israel uwe mzuri, sababu zilizofanya uwe mbaya ni zipi? Je sababu hizo sasa si za msingi tena? Israel inaheshimu haki za Wapalestina? Soma habari hiyo hapa.

Sunday, October 16, 2005

Makala Mpya ya Padre karugendo

Kuna makala mpya aliyoandika Padre karugendo kuhusu kumbukumbu ya Askofu Mwoleka lakini ina ujumbe mzito wa "NDOA NYOYO". Isome hapa

Thursday, October 13, 2005

Chavez kawashitukia wamisionari

Rais wa Venenzuela Hugo Chavez ambaye ni adui mkubwa wa Marekani ameshtukia wahubiri toka Marekani na ameamua atawatimua sasa. Chavez ambaye Marekani inashinikiza kuondolewa kwake madarakani anahisi wahubiri hao ni wale wale wapiga propaganda za adui wake. Soma hapa ujionee mwenyewe.

Monday, October 10, 2005

Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Tarehe 14/10/2005, itakuwa imetimia miaka sita tangu Mwalimu Nyerere atangulie mbele ya haki. Katika kumuenzi na kumkukumbuka mzee wetu huyu, Chuo Kikuu cha Cape Town kwa ushirikiano na Jumuiya ya Wanafunzi wa Afrika mashariki wanaosoma Chuo hiki wamendaa mhadhara Maalum wa kumbukumbu kutafakari mchango wake kama kiongozi, mwanafalsafa, mwanazuoni na mpigania uhuru na haki za wanyonge katika bara la afrika na duniani kote. Mgeni Rasmi katika tukio hili atakuwa Prof. Haroub Othman wa chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Katika tukio hilo tunatarajia tutakuwa na wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali hapa Afrika ya Kusini na wawakilishi toka balozi mbalimbali. Huu ni mhadhara wa kwanza kuandaliwa na chuo hiki na ni nia yetu kufanya tukio hili liwe la kila mwaka. Nitazidi kuwafahamisha zaidi juu ya tukio hili.

Friday, October 07, 2005

Kichaka alitumwa na Mungu

Msemaji wa George Kichaka anakana kwamba rais wake aliwahi kusema kwamba alitumwa na Mungu kuivamia Iraq na Afrighanistan kama inavyodaiwa na mwakilishi wa mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati toka Palestina Bwana Nabil Shaath. Kukana ndio kawaida ya wasemaji wote wa serikali duniani. Cha kukumbuka ni kwamba vita hizi zote huombewa kwanza na wahubiri maarufu kama vile Bill Graham. Huyu ndiye Mungu wa Kichaka anayetaka kwenda kuua wairaq. Soma habari hiyo hapa

Tuesday, October 04, 2005

Ugunduzi mpya huwa mgumu kukubalika

Jana nilielezea washindi wa tuzo ya Nobeli katika Utibabu walivyogundua kwamba vidonda vya tumbo kwa asilimia kubwa husababishwa na bakteria na matibabu yake ni rahisi yaani kutumia "antibiotics" tuu. Hawa jamaa walianza utafiti wao miaka 20 iliyopita. Walivyotangaza mara ya kwanza walichekwa sana na kuonekana ni watu wanaotaka kuleta mzaa katika sayansi. Leo ukweli umedhihirika lakini baada ya gharama kubwa ya maisha ya watu pamoja na dawa za kutibu vidonda hivyo zinazouzwa na kampuni za mabepari. Hili si tukio la kwanza; miaka mingi iliyopita ugonjwa unaoitwa "Scurvy" ulikuwa ukiwasumbua sana watu. Akajitokeza mwanasayansi mmoja akasema watu wasihangaike; tatizo la ugonjwa huo ni ukosefu wa vitamini C. Alichekwa vibaya sana. lakini baadaye ikadhihirika kwamba ugunduzi wake ni ukweli mtupu. Sasa hivi kuna mtaalam mmoja anayeitwa Dr. Mathias Rath; anapambana na mambo mawili makubwa. Kwanza anasema magonjwa ya moyo husababishwa na upungufu wa vitamini C. Anauliza kwa nini wanyama hawapati magonjwa ya moyo lakini sisi binadamu tunayapata? Jibu ni kwamba miili ya wanyama inazalisha vitamini C ambayo ni muhimu katika kuzuia matatizo ya moyo wakati miili ya binadamu haina uwezo huo. Kwa maneno mengine tunahitaji vitamini C za kutosha toka kwenye vyanzo vingine. Jambo la pili analopambana nalo ni matumizi ya vitamini na virutubisho katika kupambana na UKIMWI. Katika mapambano haya anakumbana na upinzani wa kutisha. Upinzani uliogeukia majukwaani badala ya maabara. kampuni za dawa hazitaki kusikia dawa mbadala kabisa. Wanataka kuendelea kuuza dawa zao.
Nimalizie kwa kutoa nukuu hii: "New Truths go through three stages. First they are ridiculed, second they are violently opposed and then finally, they are accepted as being self-evident". Arthur Schopenhauer

Monday, October 03, 2005

Makala nyingine za Padre Karugendo

Niliahidi kutundika makala nyingine za Padre Karugendo. Leo nazitundika kutimiza hiyo ahadi. Anza na hii inayosema "baada ya uchaguzi" kwa kutwanga hapa, halafu kuna hizi nyingine mbili nazo kuhusu uchaguzi pia. Zisome hapa na hapa. Soma nyingine anayochambua mawazo ya Kadinari Pengo kuhusu mchakato wa watakatifu kwa kubofya hapa. Mwisho kuna makala anayojadili kitabu kinachoitwa "Parched Earth" kilichoandikwa na Elieshi Lema. Kabla sijakuelekeza kwa kuisoma makala hiyo nizungumzie kidogo kitabu hicho. Hiki kwa mawazo yangu ningemshauri kila kijana akisome. Kila mzazi pia akisome. Ukikisoma utaona hali halisi ya maisha ambapo wazazi tunaacha vijana wetu wakielea bila maelekezo na mafundisho ya kutosha kuhusu maisha. Kitafute ukisome. Hutajuta kukisoma sana sana ukishasoma utataka na mwenzio akisome. Sasa uisome makala ya Padre Karugendo kuhusu kitabu hicho hapa

Bakteria na vidonda vya tumbo

Tofauti na ilivyozoeleka na kuaminika siku zote kwamba vidonda vya tumbo husababishwa kwa kiwango kikubwa na mifumo ya maisha na mfadhaiko(stress), sasa wataalam wamegundua kumbe zaidi ya asilimia zaidi ya asilimia 80 husababishwa na bacteria waitwao "Helicobacter pylori". Wanasayansi wawili toka Australia Barry J. Marshall na J. Robin Warren wamepata tuzo ya Nobel kwa ugunduzi huu. Soma mwenyewe habarii hiyo hapa. Wiki hii pia washindi wengine wa tuzo za Nobeli wa Amani, Kemia, Fizikia watatangazwa. Jumatatu ya tarehe 10/10 ndio atatangazwa mshindi wa nishani hiyo katika uchumi, huku tarehe kamili kwa mshindi katika fasihi ikiwa haijatolewa rasmi. Unaweza kusoma zaidi habari za tuzo za Nobeli hapa

KITABU CHA WAGENI