Thursday, October 20, 2005

KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI

Nimekutana na maoni ya mzalendo mmoja kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili nikaona nishirikiane nanyi kupata anachosema: maoni yake nayaweka hapa chini:
KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI
Mzee Nimejifunza yafuatayo na siyo vibaya tukichangia:
(1) Kule Mbeya, Bukoba, Moshi, Iringa na sehemu nyingi zenye baridi watu wanakunywa zaidi CHAI ya kahawa. Wakati sehemu za joto joto kama Dar hawana chaguo maalumu, hata CHAI ya siturungi, milo, cocoa,zote zinanywewa bila mpangilio wowote.
(2) Yule NYERERE wa Msumbiji aliyekuwa akiitwa SamoraMasheli alikufa kwa ajali ya ndege na wala siyo gari.Na NYERERE wa Libya, Gadafi huenda akawa ndiyekiongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu. Somali wao hawana NYERERE bado, hii ni kwa ajili yamachafuko ya kivita.
(3) Kila nchi duniani hutumia lugha ya KISWAHILI kuunganisha jamii zao za makabila mbalimbali na kufundisha katika ngazi na nyanja zote za elimu. Mfano, Uganda, Malawi, Zambia, n.k., wao hutumia KISWAHILI cha Kiingereza. Gabon, Congo, Senegal, n.k.wao hutumia KISWAHILI cha Kifaransa; England, Wales,Marekani na Scotland hutumia KISWAHILI cha Kiingereza;Misri, Libya, Tunisia, n.k. wao ni KISWAHILI chaKiarabu; Uchina nasikia ni KISWAHILI kinachoitwa Mandarin; Arjentina, Kolombia, Chile, n.k. niKISWAHILI cha Kiispania, Urusi ni Kirusi, Ureno naBrazili na Angola ni Kireno, n.k. n.k.?
(4) Nchi yetu Tanzania ambayo KISWAHILI chake ni Kiswahili, ndiyo nchi pekee duniani ambayo imetumia KISWAHILI kuunganisha watu wake wa makabila mbalimbali halafu maajabu imekataa kutumia KISWAHILI hicho hichokatika kutoa na kupokea elimu mashuleni na vyuoni mwake !!!!!!!!!!!!. Hii inamaanisha kuwa kinachofundishwa mashuleni kwetu siyo elimu bali mahudhurio ya semina ndefu ndefu tulizozibatiza majina; Form IV, IV na madigirii.Nadhani vyeti vyake sahihi vingeitwa VYETI VYAMAHUDHURIO YA SEMINA YA FORM IV, n.k. na siyo vyeti vya ELIMU. Neno elimu ni pana na kubwa. Hivyo lisitumike pasipostahili. Vinginevyo ni sawa na kudai kuendesha kilimo cha minazi wakati shamba zima umepandikiza makuti mabichi!! Na misingi ya kukataa kutoa elimu kwa KISWAHILI ndiyo chanzo cha umaskikini wetu pamoja na kuwa matajiri wenye raslimali lukuki:watu takribani milioni 40, ardhi yote yenye rutuba,maji hadi kiama - yawe chumvi au baridi, hali ya hewa murua - hakuna vimbunga-matetemeko ya ardhi-baridi na joto zinazoua, madini kila aina nchi nzima, mbuga za wanyama duniani hakuna na lugha ya KISWAHILI iliyo pevu. Nchi zote duniani zinapotoa elimu kwa KISWAHILI chake,siyo wapumbavu, hivyo na sisi tuanze leo. Anayedai lugha haijakuwa bado, mwambie akupangia lugha ya kwanza hadi ya mwisho kama ataweza, hawezi, kwani hakuna kitu kama lugha changa. Anayesema tutafsiri kwanza vitabu kutoka lugha za kigeni - muulize mbona tunatumia maneno kama motokaa, oksijeni, pasipoti,kompyuta, redio na wenzetu nao wanatumia maneno yetu kama panga, shamba, safari, kimeharibika nini?. Anayedai hatutatambulika duniani - kwanza, waulize duniani kuna nchi ngapi zisizotumia hiyo lugha ya kigeni tunayoikumbatia - na wanatambulika zaidi yetu??pili wafahamishe kiswahili kinasambaa kama moto wa mbugani. Wasikilize Wakongo, Waburundi na Rwanda,Wakenya, Wamsumbiji, n.k. wanavyokiongea. Tatu waombe wasikilize redio Ujerumani, Peking, Sauti ya Amerika,BBC, n.k. Mwisho waelimishe kuwa wanapodai kuwa lugha haijakuwa, hatutatambulika, n.k huwa wanamaanisha,tena bila kujitambua wala aibu, kuwa wao ni wanyonge,dhaifu, wasiojiamini, wasioweza kujiendesha wenyewe,watumwa - haswa haswa huko vichwani mwao na wasiotakakuelimika.
Kwaheri,
Kiswahili chema,

5Comments:

At 9:55 PM, Anonymous Anonymous said...

ama kweli huu utumwa wa matumizi ya lugha za watu utatumaliza. Tusipojikusanya na kuamua kutumia kiswahili chetu tumekwisha. Tutabaki kuwa watazamaji na washangiliaji wa maendeleo ya wengine.

 
At 12:35 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Hii lazima nirudie kusoma nikiwa nimetulia vyema. Asante kwa makala ya Prof. Othman.

 
At 9:15 AM, Blogger mloyi said...

Kiswahili, kiswahili. kila mtu anakizungumza na kote. indya jaribu kutembelea hapo top deck- kituo cha treni capetown mjini- usikilize watu wanavyoongea kiswahili na aina zake, usishangae m-xhosa kukuongelesha kiswahili!
Lakini bado wanadai siyo "academic language", . Tulipokuwa mlimani kulikuwa na mtaalamu mmoja aliletwa na uingereza moja ya hoja zake ni kwamba kiswahili hakiwezi kutumiwa kufundishia sayansi kwa sababu hakikukua na sayansi! ila kiingereza ndicho kilikuza sayansi hivyo ndiyo lugha muafaka kwa sayansi. sijui hayo maoni aliyatoa kwa kukubaliana na nani, na waliomtuma?, sijui kama shirika lake likikaa kuongea na wakuzaji wa mitaala wa Tanzania labda ndiyo jibu wanalopewa nao hulikubali!.
Kiswahili hakipendwi lakini kama mwalimu akiwa haongei kiswahili hata kidogo kwenye somo wanafunzi, wa sekondari, wanamchukia kwamba hajui kufundisha.
Hivyo tuambizane ni nani aliyekataa kutumia kiswahili.

 
At 12:23 PM, Blogger Indya Nkya said...

Hatutarajii kwamba muingereza anayetaka kuendeleza utamaduni wake kuabudiwa kwa njia ya lugha atushauri lolote zuri kuhusu matumizi ya kiswahili. Tunatakiwa sisi wenyewe tujue kwamba lugha yetu inafaa kufundishia. Tuliokataa matumizi ya kiswahili ni sisi wenyewe. Tunatakiwa tufike mahali tuanze. Hatutakiwi ushauri wa mzungu hata siku moja. Kwani kichina kimewezaje, kijapani, kimalay na nyinginezo.

 
At 4:59 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Nkya,
Sasa nimesoma vyema. Huyu bwana aanzishe blogu! Nimecheka sana. Anayosema ni kama mzaha ila ukichungulia ndani ya huo mzaha kuna mambo mengi mno.

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI