Monday, October 24, 2005

Mijadala, mijadala na mijadala

Leo nilikuwa kwenye mjadala mmoja kuhusu mambo yanavyokwenda hapa Afrika ya Kusini. Waongeaji katika mjadala ule walikuwa rais wa zamani F.W. De Klerk na mtu anayeitwa Tokyo Sexwale. Huyu Sexwale ni mweusi ambaye alikuwa kati ya wapambanaji waliofungwa miaka mingi huko Robin Island. Lakini baada ya miaka 11 tuu ya utawala wa weusi amekuwa ni tajiri mkubwa sana. Mjadala ule ulikuwa wa kufurahisha. De Klerk anasema kwamba weupe wanaogopa sana hiki kinachoitwa Black Empowerment kwa sababu hatma ya weupe haijulikani na sasa baadhi wameanza kuwapeleka watoto wao nje ya nchi wakihofia kitakachotokea kwani huenda wakatengwa kiajira na mambo mengine. Anadai pia kwamba umasikini umeongezeka licha ya uchumi kukua. Kwa mfano anasema pengo kati ya walio nacho na wasionacho limekuwa sasa zaidi ilivyokuwa kabla ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi. Idadi ya weusi wasio na ajira imeongezeka kuliko kabla ya utawala wa kibaguzi. Madai yake kwa kweli ni ya msingi hasa ya ongezeko la umasikini na kukua kwa pengo la matajiri na masikini. Hoja yake nyingine ni kwamba kuwawezesha weupe haina maana kuwapa kazi za juu au fedha za biashara hata kama hawana uwezo huo. Uwezeshaji mkubwa ni kuwaelimisha ili waweze kushindana katika soko. Hili nalo halina ubishi.
Sexwale akasema kwamba licha ya kelele zote zinazopigwa, bado weusi hawajapata chochote cha kutisha. Ametoa mfano kwamba Katika soko la hisa la Johanesburg, weusi wanamiliki asilimia 1.8 tuu ya trilioni moja ya hisa zote. Hii ni baada ya miaka 11 ya utawala mpya. Akasema pia kwamba maajabu yasitarajiwe kwa kipindi kifupi kama hiki. Kwa maneno mengine watu weusi pia wasitarajie kila kitu kitamalizika kwa miaka 11 tuu. Lakini hakutuambia yeye amewezaje kuwa tajiri hivyo kwa miaka 11 tuu.
Niliwahi kusema huko nyuma kwamba Afrika ya Kusini imeshazalisha tabaka jingine la matajiri wachache weusi ambao wanapewa mitaji ya biashara na vyeo vikubwa badala ya kuimarisha elimu kwa weusi kwa ngazi zote kwanza. Leo hii kuna mamilioni ya watoto weusi hawana madawati wala viti vya kukalia mashuleni. Badala ya kuanza kuimarisha kizazi kijacho ili kiweze kushindana na hao weupe miaka ijayo wanazalisha mabilionea wachache halafu wanaacha lundo la weusi wakiangaika pasipo kazi wala elimu nzuri. Ukisikiliza mijadala yao utagundua kazi bado ipo.

4Comments:

At 11:41 AM, Blogger mwandani said...

Weusi hawanunui hisa kwa sababu ukinunua hisa unasubiri riba kwa muda mrefu. Wengi tunapenda njia ya mkato, kadhalika elimu ya hisa haijaingia akilini. Mtu yeyote mwenye kipato kidogo anaweza kununua

 
At 9:36 AM, Blogger mloyi said...

Unajua Sexwale alikuwa maarufu sana, lakini Mandela hakupenda kumuachia kiti, hivyo alimuita akamwambia anachofikiri, sexwale akakubali, hivyo akapatiwa mkopo mkubwa sana afanye biashara na awe nje ya siasa ili kipenzi cha ANC , Thabo Mbeki, kisipate tabu kutawala nchi hiyo.
Somo kubwa sana kwa afrika, umaarufu na uongozi ni vitu viwili tofauti, kama hukubaliki kuwa kiongozi fanya kitu kingine nje ya siasa.

 
At 10:59 AM, Blogger Indya Nkya said...

Nadhani ndicho kilitokea kwa Cyril Ramaphosa pia. Unajua alishindana na Mbeki kwenye siasa za ndani ya Chama. Mbeki akamshinda kugombea urais, jamaa akaingia kwenye biashara. Sasa hivi ni tajiri mkubwa!!

 
At 1:12 PM, Anonymous Anonymous said...

Habari hii inanikumbusha kitabu cha Sauti ya Dhiki cha Mwalimu Abdilatif Abdallah na lile shairi la Vuta Nikuvute Mnazini. Namuona Badi anavyoteremshwa mnazini na kuanza kulalamika na kulia.

Hali kadhalika nakumbuka hadithi ya Grain of Wheat ya Mwalimu Ngugi wa Thiong'o. Mapambano yamekwisha wapigania uhuru wanaanza kula matunda ya uhuru. Tokyo Sexwale, Cyril Ramamphosa na wengineo sasa wanakula matunda ya uhuru: Majina yao ni kitambulisho tosha cha kuwapa uanachama kwenye klabu yoyote ya mapesa,Sura na miili yao imenawiri mpaka huwezi kuamini kwamba walikuwa mashababi hatari wa harakati za kutokomeza siasa za kibaguzi: wamekuwa walainiii, wazuri wazuri kama mabishoo wa Wenge Musica, mashavu yamevimba utafikiri wanapuliza moto, matumbo yamewatoka kama wajazito wanaokaribia kujifungua. Sasa tazama wakiwa kwenye luninga wanafanya mahojiano na waandishi wa habari wa nchi za magharibi utapigwa na butwaa na kuwachwa unajiuliza maswali usiyopata majibu.

Ngoja niseme Kiingereza kidogo, Anyway, what was the end purpose of liberation struggle? If not to have good life? At least these freedom fighters are enjoying the benefits of their struggle unlike their Tanzanian comrades who are just enjoying the benefits of the position given by Tanzanians. The Tanzanian comrades are not even into business they just inject themselves into the Parliament and Boards of Directors of companies and corporations and there they become really rich!!!

Mfini ukimshangaza sana huwa anasema "...Yritän selvittää onko se lintu vai kala?.." Maana yake "..Najaribu kutambua kama yule ni ndege au samaki.."

Mungu Ibariki Afrika,

F MtiMkubwa Tungaraza.

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI