Nashauri kila mtu apitie lile jedwali la mapendekezo ya Mramba katika kubadilisha viwango vya kodi ya mapato ya ajira. Kuna mambo mengi sana unayoweza kucheza nayo kwenye lile jedwali. Kwanza utagundua wafanyakazi wa Tanzania wanalipa kodi kubwa si mchezo. Angalia kwa mfano mtu mwenye mshahara wa shilingi 100,000 kwa mwezi, ina maana kwa miezi 12 atapata shilingi 1,200,00. Mtu huyu atalipa asilimia 18.5 ya mshahara huo kwa mwaka kama kodi. Ina maana atalipa kodi ya shilingi 222,000 kwa mwaka. Kodi yake ya mwaka inamlipa mfanyakazi wa kima cha chini kwa miezi inayokaribia mitatu. Hiki ni kiasi kikubwa cha pesa. Nadhani viwango vya kodi zetu kwa ujumla ni vikubwa kweli. Nadhani wafanyabiashara wadogo na wale wa kati wana nafuu kubwa kwa sababu viwango vyao vya kodi kutegemeana na mauzo kwa mwaka ni vidogo kulinganisha na hivi vya wafanyakazi.
Jambo la pili unaloweza kuona ni kwamba wale wafanyakazi wanaolipwa mshahara ambao tofauti yake na kima kinachotozwa kodi cha shilingi 80,000 ni ndogo wataumia sana. Mfano mfanyakazi anayepokea 90,000 akilipa kodi ya asilimia 18.5 atabakiwa na shilingi 73,500 pungufu ya kile cha kima cha chini, anayepokea 100,000 atapata shilingi 81,500 akishalipa asilimia 18.5 tofauti yake na kile kiwango kinachotozwa kodi ni shilingi 1,500 kwa mwezi. Haya mahesabu si mchezo.
Jambo jingine ninalotaka kuzungumzia ni jinsi Serikali inavyopoteza mamilioni kwa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara midogo. Kwa hali ya kawaida, waajiri wengine, wawekezaji, mashirika ya kimataifa na kadhalika yanapoajiri yanaangalia mishahara inayolipwa na mwajiri mkubwa. Kwa maana ya Tanzania, Serikali ndiyo mwajiri mkubwa. Sasa kama mwajiri mkubwa analipa kiduchu na wao watalipa mishahara ambayo si mikubwa sana, hapa serikali inakosa mapato ambayo ingeyapata kupitia hawa waajiri wengine kama wangelipa mishahara mikubwa zaidi. Hili ni suala la kisera linalotakiwa maamuzi. Sikatai kwamba mishahara pia hulipwa kutokana na tija. Kinachotakiwa ni Serikali kuangalia hili upya na kufanya mahesabu ambayo yataleta uwiano mzuri na kuongeza pato kupitia kodi zitokanazo na ajira.
Kuna haya majigambo kwamba Serikali imekuwa ikiongeza mishahara kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita kutoka shilingi 17,500 kwa kima cha chini mwaka 1995 hadi shilingi 60,000 mwaka 2004 kwa mwezi. Hapa ukiangalia tofauti utadhani ni kitu kikubwa kweli kweli na mwanasiasa anatamka tarakimu hizi akiwa ameuma meno yake kwa msisitizo. Tuambie hizo 17,500 zilikuwa zinanunua bidhaa na huduma kiasi gani mwaka 1995 na kwa sasa hizo 60,000 zinanunua kiasi gani? Huo ndio ungekuwa unyambulifu wenye akili lakini tarakimu tuu hazina maana. Kwenye uchumi tunachoangalia ni mapato yananunua nini kwa kipindi kati ya sasa na baada ya muda fulani.