Niko kwenye Basi nasafiri toka Moshi kwenda Dar. Tukikaribia Dar mjadala unaanza kuhusu uchaguzi. Ndani ya basi kuna mama mmoja mbaye niligundua baadaye sana kuwa ni diwani wa CCM huko Moshi. Mama anaanza kusomesha vijana umuhimu wa kuipigia kura CCM. Madai yake ni kwamba CCM imewalea hao vijana, pili CCM imeleta amani na tatu kwa hali ilivyo CCM imeshashinda. Vijana wale walikuwa na hasira sana kwa maneno ya yule mama wakipinga madai yake hayo. Sikupenda kuingilia mjadala ule kabisa lakini mwishoni nilishindwa kuvumilia. Sikutaka kujadili madai mawili ya CCM kuleta amani na kuwalea na kuwasomesha watanzania kwa sababu naelewa jinsi tunavyochanganya haya mambo. Mtu unaposomeshwa kwa fedha za umma watu wanafikiri nini sijuhi. Umma ndio umekulipia, ni umma umekusomesha. Serikali ipo pale kama wakala tuu. Kama huu umma haukulipa kodi serikali haitakuwepo na ni wajibu wake kuutumikia umma wote. Ikishindwa kuutumikia kuna njia za kuiondoa hiyo serikali. La CCM kuleta amani nililijadili katika makala yangu ya utamaduni wa amani(makala hii ipo kwenye kona yangu ya makala ndani ya hii blogu.
Nilianza kubisha pale huyu mama aliposema CCM imeshashinda. Mimi kama mchumi nilifikiria jinsi gharama za uchaguzi zilivyo kubwa na jinsi ambavyo umasikini umetapakaa nchini. Watu bado wanakufa kwa kipindupindu Dar es Salaam! Kwa nini sasa tutumie mabilioni kupiga kura wakati mshindi ameshajulikana? Nilimtupia huyo mama swali hili. Kabla hajajibu kuna bwana mwingine akadakia. " Wewe kama si mjumbe wa NEC hukumchagua Kikwete, lakini sisi tunajua Kikwete ndiye rais, upigaji wa kura ni formality tuu". Nikamuliza kwa nini Tanzania tusianze haka kautaratibu kazuri ambapo kila chama kikishamteua mgombea wake tunaangalia tuu wingi wa washabiki wanaompokea na yule atakayepokelewa na watu wengi ndiye awe rais tuokoe mabilioni ya kupiga kura? Jamaa akasema hapana. Ni lazima kupiga kura. " Si unaona hata mataifa makubwa kama Marekani ni lazima wapige kura?"Aliendelea yule bwana. Nikamwambia kwa nini sisi kama watanzania tusibuni utaratibu wetu ambapo mshindi atajulikana tuu kwa kutazama idadi ya wapokeaji baada ya kutangazwa na chama chake? Baada ya hapo nchi nyingine zinaweza kuiga toka kwetu. Isitoshe tuna uzoefu. Tutamuomba tuu Spika aliyemaliza muda wake atusaidie kwa uzoefu wake wa pale bungeni anapouliza: wanaokubali waseme ndiyooooo..... wasiohafiki waseme siyooooo......- Waliofiki wameshinda na kipengele hiki kimepita. Uzoefu huu utakuwa chanzo kizuri cha kutusaidia tuokoe mabilioni ya fedha za uchaguzi na kusaidia angalau uchimbaji wa visima.