Thursday, September 22, 2005

Jamani Ujambazi!!

Ujambazi umepamba tena moto. Nasikia polisi wametangaza msako kabambe. Kama kawaida utakuwa wa siku mbili tatu halafu watakaa tena mpaka vitendo vya ujambazi vizidi tena kupindukia. Sijuhi kwa nini hilo zoezi kabambe lisiwe la kudumu. Mwaka ule walivyouawa polisi ndio kampeni kabambe ilipamba moto wakakamatwa majambazi kibao. Baada ya hapo wakakaa tena mpaka sasa ndio mpango kabambe unatangazwa tena. Sijuhi utadumu kwa muda gani tena. Lakini kwa vile mapolisi wamejeruhiwa hivi majuzi tunaweza kushuhudia tena majambazi yakikamatwa na kuadabishwa kwa nguvu ya soda.
Jambo lingine ambalo linahitaji kuangaliwa kwa makini ni huu mfumo wetu wa fedha taslimu kila mara. Hii inatokana na mfumo duni wa kifedha. Kwa mfano mfanyabiashara kukaa na milioni zaidi ya mia moja kwenye duka la fedha za kigeni. Inatia shaka kama kweli ni fedha ambazo zimefanyiwa biashara jana yake. Kama ni hivyo basi ni biashara kabambe kabisa. Kama sivyo basi kuna watu wanakaa na fedha bila kuziweka benki na hilo linatia mashaka kwa sababu aidha mfumo wa benki ni mbaya au wafanyabiashara wanakwepa mambo fulani. "Cash Economy" ni mfumo mbaya na hatari sana. Fedha taslimu zinashawishi sana majambazi. Mfano wa yale yaliyotokea Dodoma nayo ni matokeo ya mfumo wa taslimu. Mtu kuchukua shilingi milioni nane kwenda kufanya manunuzi au kulipa chochote ni hatari. Simlaumu yeyote. tatizo ni mfumo wetu. Kila kitu kinahitaji taslimu. Wakati umefika kuanza kuharakisha mabadiliko ya hali hii la sivyo huu uporaji wa fedha taslimu utaendelea na kukua kwa kasi ya ajabu.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI