Wednesday, August 17, 2005

Ni nini maana ya kustaafu ?

Hili neno kustaafu linanipa shida sana. Nilidhani maana ya kustaafu ni kwamba uwezo wako wa kutoa mchango katika uzalishaji unakuwa umeanza kupungua na ndiyo maana ukifikia umri fulani ni lazima ustaafu. Kwa Tanzania umri wa kustaafu ni miaka 60. Umri huu uliongezwa miaka michache ya nyuma. Kabla ya hapo ilikuwa 55. Na umri huu hauwekwi tuu kwa maana ya kuwekwa kuna vigezo vinatumika na pengine utafiti unafanyika kabisa kutafuta umri muafaka wa kustaafu. Nadhani ukishastaafu sasa unatakiwa kufanya shughuli ambazo haziumizi sana kichwa na mwili wako, shughuli ambazo kwa kweli hazihitaji kukimbia kimbia. Ukimona mtu anastaafu halafu eti anachukua jembe kwenda kufungua shamba ujue huyo hawezi kuzalisha chochote. Utalima wakati wa uzeeni?

Kama ninachofikiria ni sahihi basi inaelekea bungeni ni mahali pa kupumzikia. Ni mahali ambapo hapahitajiki sana kutumia akili nyingi wala nguvu nyingi kwa sababu watu wengi wanaoijiingiza kwenye ubunge ni wazee waliokwishastaafu. Kwa maana nyingine mchango wao sehemu za kazi walipokuwa wakifanyia ulishapungua. Sasa unampeleka bungeni akawakilishe wananchi wa jimbo lake, akatunge sheria, akaishauri serikali nakadhalika. Hivi kutatokea chochote huko bungeni? Mimi nadhani hapa kuna kasoro kubwa mno. Kuna wale watakaosema kwamba busara za wazee zinatakiwa. Ndiyo zinatakiwa lakini si lazima iwe bungeni wana sehemu nyingine wanazoweza kupenyeza hizo busara. Pili nani alisema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya busara na uzee? Kuna kuchanganya mambo hapa. Kuna tofauti kubwa kati ya busara na kuona mambo kwa miaka mingi. Labda Kiswahili changu ni kibovu nashindwa kuelewa kama kuona mambo kwa miaka mingi ndiyo busara. Kuna vijana wadogo wenye busara kuliko wazee wa miaka 80!. Na kama hujawahi kuwa na busara udogoni mwako huwezi kuwa nayo uzeeni hata utambike.

Mimi nadhani sasa wakati umefika kwamba ukishafikia umri wa kustaafu uache zile kazi nzito na zenye kuhitaji msuli hasa msuli wa akili. Labda tukubaliane kwamba kwenye siasa hakuna kazi za kutumia nguvu na akili nyingi ndio maana ukishastaafu unaweza kujimwaga na kuanza kwenda kukaa kwenye vikao Dodoma huku usingizi ukikuandama bila kutoa mchango wa maana katika miswada inayowasilishwa. Mawaziri wazee nao huu uwe mwisho wao. Labda pia iwe uwaziri nao ni kazi ya mteremko isiyohitaji nguvu na matumizi ya akili.

0Comments:

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI