Thursday, February 16, 2006

Afrika haitaji msaada wa Chakula

BBC iliendesha mdahalo mzuri sana kati ya Nicholas Crawford toka WFP na Tajudeen Abdul-Rahem Wa Justice Afrika kuhusu chakula barani Afrika. Jamaa wa Justice Afrika anadai kwamba hakuna haja ya Afrika kupewa msaada wa chakula na anajaribu kuelezea kiini cha tatizo la njaa barani Afrika na jinsi misaada inavyolemaza bara hili. Mzungu wa WFP anatetea umuhimu wa msaada wa chakula. Kwa kweli nakusihi usome mdahalo huo hapa. Ni mdahalo mzuri mno.

Kuua Mwenzi wako ni upendo?

Nchi ya Botswana imekumbwa na ongezeko la mauaji yanayotokana na wanaume kuwaua wapenzi wao. Mwaka 2005 peke yake inasemekana kulitokea vifo sabini. Wenyewe siku hizi wanaita "Passion Killings". Botswana ni nchi ndogo- si kwa ukubwa wa eneo bali kwa idadi ya watu. Ina watu wapatao milioni moja na laki sita tuu. Halafu maambukizi ya Ukimwi ni ya kutisha. Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 40 ya watu wazima walioambukizwa. hapohapo kuna ongezeko kubwa la vifo kutokana na ajali nyingi shauri ya uendeshaji mbovu hasa kutokana na kunywa pombe kupindukia. Sasa haya mauaji ya kina dada tena inaongezea idadi ya vyanzo vikuu vya vifo yaani UKIMWI na Ajali. Ni hatari. Wanaume hawa mara nyingi wakishaua nao hujiua kwa vile wanajua watakuja kuhukumiwa adhabu ya kifo. Soma habari hiyo hapa

Wednesday, February 15, 2006

Naanza safari ya kuhama

Nimeanza kuhamia kwenye wordpress. Siku tatu zilizopita nilikuwa nashindwa kabisa kuingia kwenye blogger.com ili niweze kuandika mambo kwenye blogu. Pamoja na hayo nimepokea ushauri wa Ndesanjo kuwa wordpress inaendana na mabadiliko mapya yanayotokea kila mara. Unaweza kunisoma kwa kubonyeza hapa. Nitaendelea kuweka viungo vya blogu na mambo mengine taratibu.

Maisha yetu baada ya Miaka 50

Kwa wale wasomaji wa makala za Padre Karugendo, naweka makala yake moja ambayo aliiandika kama changamoto kwa waliofikisha umri wa miaka 50 mwaka huu. Yeye ni mmojawapo wa hao waliofikisha umri huo. Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa

NEPAD ubeberu mpya

Kuna mjadala sasa kwamba hili dude linaloitwa NEPAD ni aina mpya ya ubeberu ambapo Afrika ya Kusini inatumia kupeleka mitaji katika nchi nyingine za Afrika. Kuna bwana mmoja kaandika kitabu juu ya hili. Lakini hata kusingekuwa na hicho kitabu hili ni jambo la wazi kabisa. Ukiangalia changamoto wanazokabiliana nazo hawa jamaa wa Afrika ya kusini utagundua kwamba ni ukweli mtupu. Baada ya ule mfumo wa kibaguzi kwisha mwaka 1994 ilibidi watafute nafasi ya kuwakuza kiuchumi weusi. Njia rahisi ilikuwa ni kuwatafutia weupe nchi za kupeleka mitaji yao ili nafasi ibaki nchini mwao kuwasaidia weusi. Nchi nyingi za kiafrika zimeingia kwenye makubaliaono hayo bila kuona janja ya hawa jamaa. Tatizo ni kwamba biashara inakuwa ya upande mmoja. Nchi nyingi sana hazina mtaji wa kuwekeza Afrika ya kusini. Kwa hivyo tutawasidia kupunguza matatizo yao huku hizo sera zikiwa hazisaidii sana nchi zingine. Wanapotoka kwenda nje hawana mpango wowote wa kuendeleza nchi wanazowekeza. lao ni kupata faida na kuondoka. Ubeberu huu mpya sijuhi utatufikisha wapi.

Gregory yuko wapi?

Nilikutana na binti mmoja ambaye tulikuwa wote Jeshi la Kujenga Taifa (Ndesanjo huliita la kubomoa taifa) akaniuliza: Hivi Gregory yuko wapi siku hizi? Nikamuuliza Gregory gani? Akanishangaa akasema kumbe urafiki wenu uliishia jeshini? Nikamuuliza jina lake la pili ni nani? Akaniambia Macha. Ohh!! Nikamwambia nimemkumbuka sasa. Nikamwambia kwamba Macha alirudisha jina lake la Gregory kwa Mchungaji wake kama mmoja wa wahusika katika kitabu cha Pambazuko Gizani alivyotaka kurudisha jina lake la Paulo kwa Padre. Binti wa watu hoi. Nakumbuka Macha alipokuwa kwenye jitihada za kurudisha jina lake alikuwa akinishambulia kila siku nirudishe la kwangu pia ikiwa ni ishara ya ukombozi mpya. Kabla ya kurudisha jina lake Ndesanjo alikuwa akiitwa Gregory!!!

Ilikuwa lazima Yesu afe?

Rafiki yangu mmoja ameniacha hoi aliponiuliza kwamba; hivi Mungu alikosa njia nyingine ya kumkomboa mwanadamu mpaka amtume Mwanae wa pekee afe kwa ajili ya dhambi zetu? Kulikuwa na ulazima wa damu kumwagika? Huyu jamaa yangu yeye si mfuasi wa dini za kuja kwa hivyo nikaona kwamba pengine anauliza mambo hayo kwa ajili hiyo. Baadaye nikaingia kwenye mjadala mwingine na jamaa mmoja mfuasi mzuri wa madhehebu ya kikristo. katika maongezi yake akasema angekuwa rais wa dunia angewaua watu wa jinsia moja wanaotaka kuooana. Jamaa akambana hivi wakristo mnaua? Nikapata jibu langu la awali la kwa nini Yesu afe? Jamaa alisema ndio maana Mungu alimtuma Yesu aje afe kutoa ishara kwamba hakuna ukombozi pasipo kumwaga damu!!

Thursday, February 09, 2006

umeshasoma Makuhadi wa soko Huria?

Kama hujakisoma basi umekosa mengi. Nilikisoma mara ya mwanzo mwaka 2003 nikakirudia 2004 nimemaliza kukirudia tena mwaka huu. Chachage si mchezo. Ameandika. Ni riwaya yenye matukio yanayoendana na hali halisi ya Tanzania. Ukikisoma huwezi kushangaa kwa nini Chinua Achebe alikimbia nchi baada ya kitabu chake cha A man of the people. Alimaliza kitabu chake kwa kuonyesha kwamba jeshi limepindua nchi. Na ikapinduliwa baada ya muda mfupi. Wengi walidhani alihusika. Lakini wapi mwenyewe anasema ni kule kuisoma jamii na kuielewa. Chachage ndivyo alivyoielewa jamii ya Tanzania. Amegusa kila eneo; usanii wa wabunge; rushwa mahakamani; waandishi wa habari kuingizwa mtegoni; na mengineyo. Kitabu kina historia nzuri sana. Kuna michapo ambayo hutajutia wala kitabu hakitakuwa kirefu kukisoma. Mchapo wa mzungu kala fenesi kwa mfano au wa padre huko Musoma ambaye aliamua kumpa mtoto shilingi mia na mama shilingi 20! Soma tafadhali. Utakutana na jinsi Salama mke wa Mjuba alivyoamua kumpa mwanae jina la Mchungaji anayeombea vita huko Marekani baada ya kuokoka. Kitabu kimekamilika. Ujuhadi unavyofanywa na watu wenye nyadhifa. Elimu waliyo nayo waze wetu nakadhalika ni mambo ambayo yamesheheni ndani ya kitabu Hicho. Soma Makuhadi wa Soko Huria ufaidi.

Wednesday, February 01, 2006

Mambo mengine! sijuhi tuanzie wapi

Mimi huwa ni kipofu wa dini. Inakuwa ngumu sana kwangu kumuuliza mtu dini yake au hata kuhisi kutokana na jina kwa sababu nimesoma na watu wenye majina ya kizungu ambayowengi huita ya kikristo lakini baadaye nikaambiwa ni waislamu wengine wenye majina ya kiarabu ambayo huitwa ya kiislamu baadaye naambiwa ni wakristo. Sasa huwa sichukulii jina kama kigezo kabisa. Sasa baada ya mawaziri kutajwa hapo Januari wengi wetu tulianza kujadili sifa zao. Lakini kuna jamaa wengine wameniacha hoi sana. Wanasema; wewe huoni Wizara nyeti zote kawapa waislamu? Angalia Fedha, Mambo ya nje akataja na Wizara nyingine lakini sikutilia maanani. Nikamuliza? Hivi Wizara kuwa nyeti maana yake ni nini? Au kwa mfano Kikwete alipokuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje kwa miaka kumi ambayo ni moja ya wizara nyeti kutokana na hao wanaodai hivyo waislamu walifaidi nini? Nilishangaa nikagundua kwamba kuna safari ndefu. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kwamba Tanzania ina asilimia 35 ya ambao si waislamu wala wakristo. Hawa watapewa wizara ipi? Na hizo takwimu za wakristo na waislamu pwngine zinafuata majina na nyingine ni za zamani. Kwa mfano kuna maelfu ya watanzani wenye majina ya kikrito na kiislamu(kama yapo) ambao hawako kwenye hizo dini au walishajiondokea na kujichukulia ustaarabu wao. Tukiendelea na huu uhayawani tutafika mahali kila dhehebu litake kuwa na waziri. Na kuna madhehebu karibu 400 ya kikristo tuu Tanzania. Sijuhi itakuwaje. Lakini hao ambao hawako kwenye hizi dini mbili nani atawawakilisha? Ndesanjo kaongelea kiapo kwa kutumia vitabu; kitukufu na kitakatifu. Suala linarudi niliyowahi kusema huko nyuma: elimu ya dini

KITABU CHA WAGENI