Wednesday, February 01, 2006

Mambo mengine! sijuhi tuanzie wapi

Mimi huwa ni kipofu wa dini. Inakuwa ngumu sana kwangu kumuuliza mtu dini yake au hata kuhisi kutokana na jina kwa sababu nimesoma na watu wenye majina ya kizungu ambayowengi huita ya kikristo lakini baadaye nikaambiwa ni waislamu wengine wenye majina ya kiarabu ambayo huitwa ya kiislamu baadaye naambiwa ni wakristo. Sasa huwa sichukulii jina kama kigezo kabisa. Sasa baada ya mawaziri kutajwa hapo Januari wengi wetu tulianza kujadili sifa zao. Lakini kuna jamaa wengine wameniacha hoi sana. Wanasema; wewe huoni Wizara nyeti zote kawapa waislamu? Angalia Fedha, Mambo ya nje akataja na Wizara nyingine lakini sikutilia maanani. Nikamuliza? Hivi Wizara kuwa nyeti maana yake ni nini? Au kwa mfano Kikwete alipokuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje kwa miaka kumi ambayo ni moja ya wizara nyeti kutokana na hao wanaodai hivyo waislamu walifaidi nini? Nilishangaa nikagundua kwamba kuna safari ndefu. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kwamba Tanzania ina asilimia 35 ya ambao si waislamu wala wakristo. Hawa watapewa wizara ipi? Na hizo takwimu za wakristo na waislamu pwngine zinafuata majina na nyingine ni za zamani. Kwa mfano kuna maelfu ya watanzani wenye majina ya kikrito na kiislamu(kama yapo) ambao hawako kwenye hizo dini au walishajiondokea na kujichukulia ustaarabu wao. Tukiendelea na huu uhayawani tutafika mahali kila dhehebu litake kuwa na waziri. Na kuna madhehebu karibu 400 ya kikristo tuu Tanzania. Sijuhi itakuwaje. Lakini hao ambao hawako kwenye hizi dini mbili nani atawawakilisha? Ndesanjo kaongelea kiapo kwa kutumia vitabu; kitukufu na kitakatifu. Suala linarudi niliyowahi kusema huko nyuma: elimu ya dini

14Comments:

At 7:29 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Nakumbuka uliwahi kuongelea hili suala la elimu ya dini. Ukasema kuwa tatizo la vipindi vya dini shuleni ni kuwa havifundishi juu ya dini mbalimbali bali vinafundisha wanafunzi kuhusu dini zao. Yaani muislamu atakwenda kujifunza kuhusu uislamu na mkristo kuhusu ukristo (wakati ambapo kuna madrasa, kipaimara, mafundisho, sande skuli, n.k.). Hoja yako ni kuwa vipindi vya dini vitumike kutufunza juu ya dini alizonazo mwanadamu. Nilikubaliana nawe wakati ule na leo ninakubaliana nawe. Elimu yetu ya dini ni finyu sana. Inaanzia kwenye ukristo na kuishia kwenye uislamu. Zaidi ya dini mbili hizo ni sifuri. Tena hata dini mbili hizo tunazijua kijuujuu tu.

Ningependa kuongeza kwenye hoja yako ya leo. Ukichunguza taifa letu linavyokwenda, nyimbo tunazopenda na kusikiliza redioni, maneno tunayotumia mitaani, utendaji wa kazi, maadili, utu, yanayofanyika usiku kwenye mabaa na gesti (ambazo wanaokwenda huko sio wageni ingawa zinaitwa nyumba za kulala wageni), rushwa, mauaji ya vikongwe, ujambazi, upigaji mawe hadi kuua wanaodaiwa majambazi, n.k. utagundua kuwa asilimia ya wakristo na waislamu ni ndogo sana. Huenda, kama nimekosea Nkya nisahihishe, Tanzania hakuna mkristo au muislamu hata mmoja!
Au pengine wapo ila dini hizi zimeshindwa kufanya kile kinachodaiwa katika mafundisho yake.

 
At 6:30 PM, Blogger mloyi said...

Mgawanyiko unaendelea, baada ya kuangalia huyu jamaa atalisaidiaje taifa sisi tunashupalia yule jamaa ni wa dini fulani na yule ni wa dini ile.
Watu wa dini hao kaka ndesanjo! ndiyo tabia zao zilivyo, wanachojali ni kuona kwamba dini zao zinazishinda nyingine, hata kwa hila ambazo wanaongelea kila siku kwamba mungu au Mungu(sijui tofauti yake) anazichukia. Ni mbwa mwitu ambao huvaa ngozi ya kondoo waendapo kusali, lakini hawatimizi mapenzi ya miungu yao. Angalia wanaochukua rushwa na wengine wa staili hii, ndesanjo ameshawasema wote,. kwao la maana ni biblia na korani.

 
At 7:50 PM, Blogger Egidio Ndabagoye said...

Watanzania tuache unafiki! hivi yule anae kula rushwa ya 10% ni dini gani? yule anaeshindwa kutimiza wajibu wake kazini ni dini gani?.

 
At 7:23 PM, Blogger Boniphace Makene said...

Tena utasikia pia suala la huyu si muislamu safi ama huyu kafiri tu. Hizi hoja zisizo na mashiko zinaudhi na zinadumaza umma sana.

 
At 3:28 AM, Blogger Jeff Msangi said...

Nkya,
Hoja muhimu sana hii na naona wachangiaji wote wameweka msimamo wa hitaji la marekebisho ya elimu ya dini.Unajua nilishawahi kujiuliza hivi mimi na pengine wewe ningekuwa nasema dini yangu ni kadha wa kadha endapo nisingezaliwa na kujikuta nikiambiwa habari za msikitini au kanisani?Dini za mapokeo zina madhara makubwa sana,mojawapo ni la kutokuelewa kwamba kwanini wewe unaamini dini fulani na wakati huo huo kujivalisha kitambaa cha giza kuhusu dini mbalimbali zilizopo duniani.Ukichunguza kwa sana mambo haya ya dini ni ubatili mtupu.

 
At 8:32 PM, Anonymous Anonymous said...

Naam,

Kuna siku nilituma barua pepe iliyokuwa na kichwa cha habari ya Mungu Ibariki Afrika. Katika barua pepe hiyo niliambatanisha habari za waziri mmoja Kenya aliyekataa madaraka ya uwaziri kwa sababu wizara yake haikuwa nyeti!
Niliposoma habari hiyo nikakumbuka habari moja alinisimilia jamaa mmoja niliyekuwa nikiishi naye nyumba moja wakati nilipokuwa nasoma. Huyu jamaa yangu alikuwa Mkenya, alinismulia habari za waziri mmoja huko Kenya aliyekataa uwaziri kwa sababu alikuwa kashushwa cheo toka uwaziri wa fedha kupelekwa uwaziri wa Afya. Nikamsikiliza huyu jamaa halafu nikamwambia "..lakini wewe unasoma mambo ya afya..Unajiona ni duni zaidi ya mtu anyesomea biashara?.." Akanijibu "..Hapana..Lakini wizara ya fedha ni muhimu kuliko wizara ya afya.." Nikamwambia "..Hapo ndipo tunapokosea kuelewa MAANA..Na kutokana na kutoelewa kwetu ndiyo sababu tuna matatizo mengi..Haya niambie katika dunia hii yenye magonjwa mengi kama yalivyo kwa nini wizara ya afya siyo muhimu?..Hawa wenzetu huku kila wizara kwao ni muhimu na ina MAANA ndiyo sababu hiyo wizara ikaundwa.." Mazungumzo yetu yakageuka kuwa mabishano. Tukabishana sana mwishowe nikamwambia "..Basi wewe endelea kuamini unavyoamini na mimi nitaendelea kuamini ninavyoamini.."

Huku kutoelewa MAANA ndiko kunakofanya mambo mengi sana yakwame au yaishie kuwa ya chini. Kwa mfano, pale nyumbani Tanzania ninaweza kusema wizara ya Utamaduni na Michezo ni moja ya wizara inayozalisha pato kubwa sana la taifa. Ukichukulia michuano ya ligi kuu ya kandanda pekee yake inazalisha pesa nyingi sana, bahati mbaya sina takwimu kamili ya pesa zinazozalishwa na ligi hiyo lakini nina hakika ni mamilioni ya shilingi yanaingia kila siku za mechi za ligi kuu. Lakini wizara hii haina mikakati ya nguvu ya kukuza na kuborehsa kandanda. Kilichokuwa chama cha soka (FAT)Tanzania kilikuwa hakina taarifa zozote za kufurahisha. Ulikuwa ukisikia neno FAT linakutia karaha kama maana yake kwa Kiingereza. Hebu tujiulize mataifa ya Kameruni na Naijeria yanapata kiasi gani cha fedha za kigeni kutokana na wachezaji wake wanaocheza soka ya kulipwa ughaibuni? Nikiendelea na wizara hiyo hiyo tujiulize taifa limekuwa linaingiza kiasi gani cha fedha kutokana na kodi inazopata kutoka kwenye bendi za muziki wa dansi, taarabu, na ngoma za kiasili? Nina hakika kila usiku mmoja Wizara ya Utamaduni inapata fedha nyingi sana kutokana na shughuli starehe ya muziki. Lakini hapo hapo Tanzania haikuwa na studio za kufyatulia santuri! Kile kiwanda cha kufyatulia santuri pale Kijitonyama kilififia kimya kimya. Chukulia mfano,Afrika ya Kusini inaingiza kiasi gani cha fedha kutokana na shughuli za muziki? Tanzania tungekuwa tunaingiza mabilioni ya fedha kutokana na muziki. Ninasema hivyo kwa sababu kwanza muziki wa Tanzania ulikuwa na ghani (peculiar melody) yake yenyewe na hiyo ni moja ya kipusa ambacho kingeuuza muziki wa Tanzania ulimwenguni kote. Sitaki kuchukulia mifano mikubwa kama ya wanamuziki wa Marekani ambao ndiyo mabalozi wakubwa wa vijana dunia kote. Leo hii ni kitu aghalabu na adimu sana kukuta nyumba ambayo haina muziki wa Kimarekani au kusikiliza radio yoyote duniani bila kusikia miziki ya Kimarekani. Na kwa kwa juhudi za kitaifa dunia nzima imechotwa na muziki wa Wamarekani ikiwemo Tanzania na hiyo mikelele ilioenea kwa jina la Bongo Fleva.

Ni muhimu kwete sote kutambua umuhimu wa wizara zetu na kuzifanyia kazi katika umuhimu na MAANA zake kamili. Tukifanya hivyo tutaendelea upesi mno. Tukifikia hapo hatutasema tena ili tuendelee twahitaji vitu vinne; watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora. Tutasema ili tuendelee twahitaji AKILI YENYE KUELEWA MAANA. Halafu tutajipangia mikakati (milestones) Halafu tutaanza kwenda na nguvu mpya, ari mpya, na kasi mpya kuelekea tulipopanga. Kwa sababu nguvu mpya, kasi mpya, na ari mpya bila kujua tunakokwenda ni sawa na mtoto aliyeanza kutambaa huwa anakwenda tu lakini hana safari maalumu.

Nikirudi kwenye suala la majina. Miye zamani nilikuwa nafikiri jina Saidi au Juma ni majina la Kiislamu na jina Charles au Pancras ni ya Kikristo. La hasha! nikajakubaini kwamba jina Charles halimo hata kwenye Biblia na wala Saidi na Juma siyo majina ya Kiislamu. Cha ajabu katika kuzurura kwangu kote ughaibuni sijawahi kukutana hata na Mwarabu mmoja anayeitwa Juma isipokuwa Juma wamejaa tele Tanzania. Halafu sijawahi kukutana hata na Mkatoliki mmoja toka Ireland au Italy anayeitwa Charles au Carlos. Zanzibar kuna Waislamu wengi sana wenye majina ya Kizanzibari kama kina Pandu, Makame, Machano, Faki nk. Ukisikia majina yao huwezi kujua ni dini gani lakini ukiangalia vichwani mwao utaziona baraghashia ndiyo zitakazokuambia kwamba ni Waislamu. Hali kadhalika huko Mbeya kuna akina Anyitike Mwalusamba huyu huwezi kujua kama ni Mkristo au Muislamu mpaka ifike Jumapili au Jumamosi anapoenda kusali au kupiga mayowe madhabahuni kwake.

Jingine Wizara apewe yeyote Mkristo, Musilamu, Muhindu, na muamini imani nyingine yoyote la msingi awe na uwezo wa kuiongoza.

Namalizia kwa kuwatakieni sikukuu njema ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Kilipozaliwa chama hiki niliimba kwaya uwanja wa Taifa. Nimemkumbuka rafiki yangu mmoja ambaye tuliimba naye kwaya hii yeye sasa hivi mbunge wa CCM. Namshukuru MUNGU kutuletea vyama vingi kwa sababu siku ya leo 05.02 ingekuwa hekaheka za maandamano na magwaride na kusikiliza hotuba za wakuu wa CCM. Ingekuwa ndiyo siku ya kuvuna mapesa toka kwa wananchi, makampuni, na mashirika ya umma ili kufanikisha shamrashamra za kuzaliwa kwa CCM.

Kila la kheri kwenu nyote,

F MtiMKubwa Tungaraza.

 
At 11:11 AM, Blogger Reginald S. Miruko said...

Mimi nadhani aliye safi ni yule asiye na dini. Maana ubongo wake haujachafuliwa na imani--Mabyo mtalaama mmoja alisema ni hatua ya juu kabisa ya ukichaa. Unaamini nini ambacho wewe binafsi hujawahi kukiona na hakuna mwenzio hata mmoja aliyewahi kukiona! ukichaa. ukiachana na ukichaa huo, unakuwa safi, unachodaiwa pekee ni kuwatendea wenzio kama wewe ambavyo ungetaka kutendewa. BASI!

 
At 4:07 PM, Blogger Bwaya said...

Rejeo langu liwe mistari ya ufahamu ya Ndesanjo inayokwenda kwa jina la "Yesu/Isa na Watanzania" ambayo kimsingi ina mafundisho mazito.

Niliposoma mistari hiyo, nilikubaliana naye kuwa katika Tanzania wenye dini(kikweli kweli) watakuwa ama ni wachache sana ama hawapo kabisa kama alivyorudia kulisema hilo katika mchango wake hapo juu.

Huo ndio ukweli. Yaliyobaki ni unafiki mtupu, mtu nadai ni Mkristo na eti anashikilia mafundisho ya Yesu wakati anayoyafanya ni tofauti kabisa na maneno yake.

sijui kama itakuwa sahihi tukikubaliana Reginald Simon (mkristo?)kwamba afadhali asiye na dini!...nahisi ni afadhali kwa sababu alizozitaja.

Lakini swali linakuja: Dini zipo na hazishikwi, zinaaminiwa kijuu juu. Je zisingekuwapo, si ingekuwa ni balaa zaidi? Si afadhali hata wazuge zuge?

 
At 3:04 AM, Blogger John Mwaipopo said...

Ukisikia wa-Afrika tuko njia panda ndio hapa. Hata wakati wa 'Mtakatifu' Nyerere matatizo haya yalijitokeza sana. Hizi imani tulizopandikizwa na wazungu na waarabu zinatuparaganya sana. Nadahni wakati umefika sasa tuzipige teke mioyoni mwetu. Hivi hao 35% ndio tuseme hawana Mugnu, Mimi nafikiri wanaye.

Lililopo Tanzania ni mbegu ambayo kwa upofu fulani hivi ilipandwa na wakoloni ya watu wa majina (sio dini)fulani kupata manufaa fulani na watu wa majina tofauti kusahauliwa au kuenguliwa kwa makusudi. Yafaa basi ili kujenga umoja tujipofushe na dini na tukodolee mambo yanayohusu maendeleo yetu.

 
At 10:52 AM, Blogger Indya Nkya said...

Si kwamba hiyo asilimia 35 hawana dini. Wana dini zao za asili na wanaabudu ni kwamba hawana dini za mapokeo za kiislamu na kikristo

 
At 7:21 PM, Blogger mark msaki said...

Kwa kaka Nkya tunashukuru kuleta mjadala, kaka Tunga nimekubali uchambuzi wako ni sahihi....kama kilivyo kilio changu safari hii umeanzia ndani, tusafishe halafu ndio tuende nje!!!maana kama sisi hatutaki kuuza wachezaji wetu na kufanya mambo proffession, wao si ndio wanafurahia kuchukua vinavyoelea kiulanini????

ni kweli kabisa, hatujui maana...nyerere akasusa kwenda nashno stadium, miziki ikawa inaburudisha wahishimiwa baada ya mikutano, sanaa au kipaji kilifanywa cha kujitolea, .......vipaji au sanaa vikawa sio tena njia halali ya kujipatia riziki ila ni shughuli ya kufanya baada ya kazi kwa ajili ya kujenga afya.........

watoto wakaenda shule, wazazi hawataki kusikia mambo ya michezo sanaa...kwani nani asiyejua wasanii, na wanamichezo hujifurahisha...nani asiyependa kufanya kazi serekalini??? au kuajiriwa??? ushinde ukiburudisha??? nani aliyeona mtyu kafanikiwa kupitia michezo?? huko nje lakini sio hapa nyumbani....soma kwa bidii utacheza ukiwa na kwako...haya ndio usia toka kwa wazazi ambao siujutii sana mimi kama mimi lakini ni hasara kwa taifa.....

wakasoma wakapata kazi wamekariri michezo sanaa uhuni kupoteza muda, ni kweli wazee walisema jamaa kazi yao kubomu fegi sisi tuliosoma utawala na fizikia mambo safi tunafanya shughuli halali inaingiza kipato..sio wale wale wamelost...tena uhuni hata mtoto wangu hataenda huko.....nimekariri hilo......

tulio serekalini / ajira rasmi tuna sheria sisi ndio miungu watu waliobaki wadudu ndio kwani nini nani anataka kiwanja...si atoe hela (aongee vizuri)wakati tunasoma alikuwa wapi?? nani anadai kuwa muziki mpira na sanaa unaweza kuwa kazi hadi urasmishwe...kwani magabacholi wameishiwa??? hadi kuwafuatilia na sijui hatimiliki?? waapi bwana ndio faida za kusoma ...tena serekalini ndio kuzuri zaidi kinachomata hapo ni dawati ulilokalia ...usijali sana mambo ya fenicha hata kama ni dawati kama la darasa la kwanza...kinachomata hapo si ni nafasi hujui ...hata kama ukienda huko ajira binafsi hata kama ni milioni unalipwa mimi na elfukumi yangu nitakutoa knock out tu...usicheze na sisi serekali si ndio wenye nchi??? mwisho wa siku bia nitaitwa mtu wa maana tu kwani unaonaje mshahara mdogo lakini ninamiliki VX!!!!

hawa wengine wanalia imekuwa tabu kufungua biashara kwani tatizo ni nini?? kama kile kimama kilikuja hapa juzi..eti kinanisubiri masaa manne..mie nimeenda kunywa supu ya kitimoto...hawa watu wengine bwana kwani yeye masaa manne si angefanya mambo ya maana tu ananisubiri mimi...watu wengine bwana.....

sekta rasmi ikafa.....vyama vya michezo vikawa ni personal enterprises...kama hii FAT nani alisema ni mali ya mtu mmoja??kichefuchefu sitaki hata kusikia....bora wamebadilisha ikawa TFF...lakini kuna myinyo wa zamani imebadilika chupa tu...ukiwa huko hufuatwi hata kama ulitoka serekalini kwa kashfa kubwa ....ndio haijali hata kama ilikuwa ni kuuza nyara...au hata kama walipoteza watu maisha....ukienda huko hata serekali ni aku!!! haikugusi....huko ni kwenu, wizarani ni kwetu....je nani anajua kuwa miss Tanzania anawajibika kwa nani?? mahesabu yao yanapitia wapi?? je wanalipa kodi halali??? hizo zawadi wanazotangaza kutyoka hewani wanazo kweli nani anawaaudit?? kama hawataki na si waache kujiita jina Miss Tanzania? je wachezaji mikataba yao je??? je mapato ya uwanja wa taifa nani anajua yanapoenda?? je mfumo wa kukata tiketi ukoje?? je serekali haiibiwi?? namna hii tutajenga uwanja mungine na mungine na mungine au fweza itaishia hewani?? je hawa vijana wa bongo flava wanaingiza kiasi gani? je hakitoshi kutoa kodi kubwa tu kwa serekali?? je tutaendelea kwa namna gani kwanini hatuwasaidii ili na sie tufaidike?? je ! je ! je! jeEEEEEEEEEEEE!!!!!!

hii wizara ya UTAMADUNI NAONA WALAAAAAAAAAA HATA MPANGO HAINA!!!!!!! JAMANI WENYE SAFU ZA MAGAZETI MUWAAMSHE SASA WAFANYE KAZI WAACHE UPUMBAVU!!!! - HII NI WIZARA AMBAYO ILITAKIWA ITENGENEZE HATA KAZI MILIONI PEKE YAKE KWA MWAKA

methali ya kiswahili ilisema asiyejua maana haambiwi maana...je tunaojua maana tusiwaambie wenzetu??

alhamsiki

 
At 11:52 AM, Anonymous Anonymous said...

Mark na wengine,

Kwa sababu ya kuwiana sana majadiliano haya na yale ya kule kwa Michuzi ninadurufu maoni niliyoyaandika kwa Michuzi ili kuongeza hoja katika majadiliano haya kwa kurejea hoja ya Mark.

SANTURI INACHEZA UPANDE WA KWANZA
Mark, uliyosema ninayaafiki kwa kila hali. Miye kwa sababu ya uchechefu wa msamiati huwa naita kukosa kujua MAANA. Viongozi wa kisiasa wa Tanzania huwa wanaona soka kama mchezo wa wanaume ishirini na mbili wanaokimbizana na kukimbiza mpira kwa dakika 90. Halafu huwa kuna refari akisaidiana na washika vibendera kuhakikisha kwa hawa mashababi ishirini na mbili hao hawaumizani. Kwa hiyo soka kwao ni burudani ya baada ya kazi siku ya Jumamosi kuanzia saa kumi na dakika kumi na tano jioni. Shughuli yoyote ya maana hufanywa asubuhi mpaka adhuhuri, au alasiri, au jioni. Ikiwa ndivyo hivyo basi kwanini wachukue muda wao kumakinikia jambo la dakika tisini tena Jumamosi jioni?!

NAIPINDUA SANTURI UPANDE WA PILI
Soka huchezwa na mashababi 22. Kumi na moja toka kila upande. Huchezwa na wachezaji kumi na moja toka kila upande. Wachezaji hao hutumia viungo vyote vya mwili isipokuwa mikono. Huchezwa kwenye eneo la mraba la mita mia nne. Kama ilivyo kawaida ya makundi yoyote yawe ni vyama vya kisiasa, wafuasi wa imani za kidini, na kadhalika huwa yana wafuasi wake hali kadhalika soka. Kwa hiyo Inapochezwa soka huwa si wachezaji ishirini na mbili wanaoshiriki huwa kuna kundi kubwa la mashabiki wa timu hizo wanaoshiriki. Mashabiki hawa huwa pengine wapo uwanjani, au majumbani au vilingeni wakishiriki kwenye pambano kwa kusikiliza radio, au majumbani au migahawani wakitazama pambano kupitia kwenye luninga. Ushabiki wa soka unaweza kuwa ni maradhi mabaya yasiyotibika. Kuna mashabiki wa soka ambao wamewahi kufikia hatua ya kujiua pale timu wanayoishabikia iliposhindwa. Kuna wengine ambao wamepoteza mali zao kwa kualifia (betting) matokeo ya mapambano ya soka. Kuna wengine waliouawa au kujeruhiwa na mashabiki wa timu pinzani. Na wapo waliopoteza urafiki na hata wapenzi kwa sababu ya kushabikia soka.

Wacheza soka ni wa kulipwa ni watu wanaopata vipato vikubwa kuliko marais, wabunge, na viongozi wengine wa kisiasa, au wanataaluma walioenda kwenye taasisi mbali mbali za elimu kwa miaka zaidi ya nusu ya maisha yao! Soka ni moja ya ajira inayotengeneza mamilionea vijana kwa kazi halisi yenye kipato halisi. Soka ndiyo kazi pekee inayoweza kumlipa mtu asiyejua kusoma wala kuandika mamilioni ya fedha kutokana na uwezo wake wa kulisakata kabumbu.

Pambano la soka ni shughuli ambayo inaajiri na kutoa vipato kwa njia mbali mbali na kwa watu mbali mbali. Kwa mfano, pambano moja la soka la ligi ya daraja la kwanza huleta vipato kwa wachezaji, wenye njia za usafiri, nyumba za wageni na mahoteli, wenye migahawa ya chakula, kwa makampuni ya vinywaji baridi, makampuni ya habari kama radio, luninga na magazeti, wauza makabrasha(merchandise), makampuni ya usalama na polisi na FFU, wauza petroli na dizeli, makampuni ya umeme, simu, telegramu na kadhalika. Halafu kuna pato kubwa linaloenda ofisi ya kodi mapato. Pato hili huwafaidisha na wananchi wengine ambao siyo mashabiki wa soka!

Katika somo la sosiolojia kuna kipengele cha sanaa na michezo kama taasisi za jamii. Hiki kipengele kinasema kwamba michezo ni kigezo kinachoonyesha afya, mpangilio (how organised or disorganised), nidhamu, na uwezo kufanya mambo kwa pamoja kwa watu wa jamii inayohusika (coordiantion). Kwa mantiki hiyo na kuwaangalia kina Mohamed Chuma na wenziye wakiwa vifua wazi tunaweza kuijadili vipi jamii yetu ya Tanzania?

Naona ule ugonjwa wangu wa mawazo kupandana unaanza tena. Akilini imenijia picha ya Mohamed Chuma akiwa na bendera ya Tanzania akizunguka uwanja wa taifa kuaga rasmi kustaafu kucheza namba tatu timu ya taifa baada ya kuitumikia kwa miaka kumi! Namuona Hayati Mohamed Kajole akiirithi nafasi Mohamed Chuma. Namuona Hayati Mohamed Kajole pale ofisi za BIMA Mtaa Samora akiwa mtu mwenye furaha saa zote ulipokutana naye. Inanijia pia picha ya Kocha Mohamed Msomali akiwa kavaa kanzu yake nyeupe karibu na jumba la sinema Sapna, mtaa wa reli Morogoro. Naona ofisi za mamlaka ya tumbaku na wachezaji aliowazalisha Kocha Msomali wakiwemo Charles Boniface Mkwasa, Zamoyoni Mogellah (kama sikosei ndiye mshambuliaji aliyepata kufunga magoli mengi kuliko mwingine yoyote katika historia ya ligi kuu ya Tanzania) Omar Hussein, golikipa Hamad masarakasi, na wengineo. Naliona jiji la Morogoro. Naona makao makuu ya timu ya Mseto, Zaragoza, na Aston Villa. Ninamuona Beki mashuhuri na sanifu sana Kocha Kido Simkoko. Nakumbuka siku nilipoimba na Cosmas Chidumule na kundi zima la wana Matimila ukumbi wa Bwalo Morogoro nilipomaliza kuimba Kocha Kido Simkoko alipokuja kunipa mkono na kuniambia "..Sikujua kama una kipawa cha kuimba, safi sana.." Mawazo yangu hayajakaa sawa, nasikia huzuni.

F MtiMkubwa tungaraza.

 
At 2:32 PM, Blogger mark msaki said...

nashukuru kwa mjadala....sasa naona bado kidogo meli itaenda sawa....umenifurahisha mzee mzima Tunga...kumbe na wewe umekaa kaa jiji kasoro bahari..kwa kina mkude na wengine....

bado hatujachelewa, mawazo yatakaa sawa tu punde si punde...jambo zuri au la maana huanzishwa si lazima na kijiji au taifa zima ni mtu mmoja....akauza sera ZAKE WAKAMUUNGA MKONO IKAKUBALIKA IKAWA SHERIA.... na siku hizi inawezekana kupitia hata taasisi zisizo za kiserekali....nadhani sasa ndio wakati, la kama tanzania ya sasa bado haitaki manabii watuue kama walivyoua waliotangulia...

cheers

 
At 10:03 PM, Anonymous Anonymous said...

Mark,

Asante kwa changamoto.

Nimepata kuishi kwenye mji kasoro bahari. Ni mji mzuri sana kwa sifa za watu wake, historia, mandhari, na hali ya hewa yake.

Naipenda Morogoro,

F MtiMkubwa Tungaraza.

 

Post a Comment

<< Home

KITABU CHA WAGENI