Kiswahili kitolewe utumwani kwanza
Jeff Msangi kaanzisha mjadala wa kiswahili katika blogu yake. Ametoa hoja za msingi ambazo zaweza kujadiliwa. Ili mjadala ule unoge naongezea makala iliyoandikwa na Prudence Karugendo anayetoa hoja kwamba tuanze kukitoa kiswahili utumwani kwanza. Hoja yake ni kwamba kiswahili kimeazima maneno mengi sana ya kiarabu wakati tuna lugha kwa mamia za kibantu ambazo tungeweza kutumia maneno yake na kubadilisha mengi ya kiarabu. Soma makala yake hapa na mjadala uendelee.
7Comments:
Lazima kwanza nikiri kwamba Karugendo amenikumbusha jambo ambalo ni muhimu na pengine nilikuwa naliangalia juu juu.Nakubaliana naye kwa asilimia nyingi kwamba kukitoa kiswahili utumwani ni msingi muhimu sana.Sijafanya uchunguzi wa kutosha juu ya uundwaji wa lugha na sina uhakika kama tunazo rasilimali za kutosha kusukuma hoja hii ila napendekeza tuinge mkono.Hapo ndipo ninaporudi kwenye hoja ya makala yangu kwamba tujivunie kwanza tulichonacho halafu kama anavyosema Karugendo tukibinafsishe,tukutilie rutuba na kukipa sura mpya.Ahsante Nkya kwa waraka huu.
Hoja hii imenifikirisha sana. Nimefurahi umeizua. Naomba muda nifikiri.
Siku zote hakuna hoja mbaya inayotolewa wazi kwenye kadamnasi. Hata mtoa hoja akiwa na malengo mabaya, ile hoja anayotoa nje huilemba iwe nzuri machoni na kwenye fikra za watu. Iwe ni utandawazi, haki za binadamu, jenda na chochote kile. Tatizo letu kubwa ni kukosa kuelewa na kutoa kipaumbele kwa hoja husika. Suala la kutoa kiswahili utumwani ni nyeti lakini siyo wakati wake huu kwani sintaliweza hilo kabla mwenyewe sijajitoa utumwani. Jina langu Jeremy/George/Crazy G/Lady X, shuleni nasoma kwa kiingereza, utumwa mkubwa kulikoni, nitatoaje kiswahili utumwani?. Suluhisho ni watanzania kujitoa utumwani kwanza halafu hii mijadala yote haitakuwepo. Chanzo cha hii mijadala ni utumwa tulio nao kwani umuhimu wa kiswahili au matumizi ya kiswahili katika elimu siyo masuala ya mijadala tena. Lugha yenyewe imetokana na biashara kati ya Wabantu na Waarabu, kuna kosa gani maneno ya Kiarabu yakiwemo. Ndiyo maana hata Msukuma anaita uje wa ndizi na nyama MTORI kwani siyo asili yake, na sisi tunaita hizo nyota pepe SETELAITI maana siyo asili yetu. Kukiboresha kiswahili kiwe ni cha Kibantu inaleta maana lakini siyo kipaumbele dakika hizi ambazo watu bado tumefugwa. Jeff kasema tuenzi kiswahili na tujifunze lugha za kigeni!!kwa madai kuwa waajiri wetu ni wageni. Bila utumwa tungeelewa kuwa sisi ndiyo tumewaajiri wale wageni nchini kwetu. Wakisema siye masikini tunakubali, wakisema wametuajiri tunakubali. Hii mijadala yote inaonyesha ni kiasi gani sisi wenyewe tulivyo bado watumwa. Umuhimu wa kiswahili na matumizi ya kiswahili si suala la mjadala kwa watanzania, labda wageni. Na kwa watoa hoja tunomba suluhisho badala ya mijadala, kwa kuanzia suluhisho langu ni kwamba: Kiswahili ndiyo kiwe lugha ya kufundishia. Watu wataelewa zaidi na upeo wao utaongezeka na hii mijadala haitakuwepo. Badala yake tutajadiliana jinsi gani tuondoe malaria, ukimwi, njaa na jinsi gani maji yafike vijiji vyote na machungwa yasiozee Dar wakati Kigoma, Singida hayapo, na jinsi gani Mwanza, Bukoba na Musoma wasikose maji wakati wanaogelea ziwani. Tuna matatizo mengi ya msingi.
Nashukuru kwa changamoto ya kutoa suluhisho badala ya mijadala. Nadhani mijadala pia hutoa suluhisho. Kimsingi hoja ya Msangi na ya anonymous hapo juu ni kutumia na kujivunia kiswahili tulicho nacho kwa sasa. Hii ni hoja nzuri na inazidi kuleta malumbano mengi sana kati ya wanaoitoa na wanaoikataa. Lakini ilivyo sasa ni kwamba kuna idadi kubwa ya watu ambao wangependa kiswahili kiwe ndicho lugha ya kufundishia ili tuweze kuwapatia wanafunzi wetu elimu bora na si vyeti.
Wanamada wanasema London ndiyo sahihi na si Landan. Ebu fikiria na hao waingereza wakiamua kutoa englishi utumwani; Arusha itakuwa Erashe, Kigoma - Kaigome, Moshi - Mushai, Lindi - Laindai, Singida - Saingaide. Nadhani katika lugha yapo majina yanayobadilika na mengine hayabadiliki hivyo lisituisumbue kichwa.
Hoja maridadi sana. Halafu suala jengine, kuna lafudhi nyingi tu za kiswahili zinazotumika kivyake vyake. tusherehekee kiswahili chetu. Namuafiki anonymous. Kwanza tuondoe ukungu kwenye fikra zetu.
Nkya na ni nani akitoe utumwani? ni mimi wewe na wengine ambao wameliona hili tatizo lakini tusitegemee eti serikali hata sikumoja au mtu kutoka nje ni sisi wenyewe na tuanze sasa.
Post a Comment
<< Home