Niliposoma takwimu za umiliki mali na mapato kati ya weupe na weusi Afrika ya Kusini nilishindwa kuamini. Katika takwimu hizo mwandishi alisema kwamba, kama ukiigawa Afrika ya Kusini kama nchi mbili tofauti; moja ikiwa ya wazungu ambao ni asilimia 14 na nyingine ikiwa ya weusi asilimia iliyobaki na ukitumia kigezo cha shirika la maendeleo la umoja wa mataifa –UNDP cha maendeleo ya watu (Human Development Index) ambapo nchi hupangwa kuanzia ya juu kabisa mpaka ya mwisho basi sura itakuwa hivi:
Taifa la wazungu asilimia 14 wanaomiliki asilimia 88 ya mali binafsi (Private Property) litashika namba ya 24 likiwa hatua moja chini ya Uhispania
Taifa la weusi ambao zaidi ya nusu wanaishi kwa kipato cha dola moja kwa siku, na asilimia 40 ya watoto wakiwa wamedumaa kwa utapiamlo litashika namba ya 123 likiwa juu ya Congo hatua moja. Hii inaonyesha ni jinsi gani pengo la walio nacho na wasio nacho lilivyo kubwa.
Nilianza kwa kusema sikuamini hizo takwimu kwa sababu ya picha ya mwanzo niliyokuwa nayo ya sehemu za katikati ya miji ambapo kuna barabara nzuri, nyumba nzuri, mahoteli makubwa, magari ya kifahari na vinginevyo. Sasa nimeamini. Nilishiriki katika utafiti wa maeneo mbalimbali ya Cape Town siku za karibuni tukiwa tunatafiti shule za Msingi. Acha utani. Maeneo wanayoishi weusi ndani ya hili jiji zuri yanatisha. Vijumba vingi ni vya mbao na mabati kote. Msongamano wa ajabu. Shule zao utaziona ziko hoi kabisa. Ukilinganisha na hizo za wazungu utazimia. Za wazungu zimesheneza acha utani. Kila kitu kipo darasani. Wanafunzi utaona tofauti zao za kuelewa mambo kabisa. Si kwamba weusi ni wajinga ila mazingira yanawafanya wasiweze kuwa kama wenzao. Tembea uone. Hapa ni mjini bado sijaenda huko vijijini nijionee.
Gazeti moja hapa siku za karibuni limetoa takwimu za kusikitisha. Inasemekana kwamba kwa sasa wanafunzi 3.6 milioni hawana viti vya kukalia na wengine milioni 4.2 hawana madawati yanayofaa kuandikia (hakuna mweupe hapa). Lakini ukiona maisha ya mijini huwezi kuamini kabisa. Kwa mtaji huu si kwamba kuna watu tofauti tuu katika nchi hii, bali pia hizi ni dunia mbili tofauti kabisa.