Thursday, January 19, 2006

Tumepoteza maelfu ya miaka ya elimu

Hivi lile Sakata la kufukuzwa kwa madaktari limeishia wapi? Kama wote walifukuzwa basi ni kwamba taifa limepata hasara ya maelfu ya miaka iliyowekezwa kwenye elimu. Tunaambiwa kwamba, kila mwaka mmoja wa elimu mtu anaopata unaongeza ufanisi katika utendaji kazi ambao hutoa mchango katika ukuaji uchumi na kuongeza maslahi ya anayepata elimu hiyo. Kwa kifupi ni kwamba rasilimali watu ni mtaji mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi. Kwa nchi yenye watu wachache wenye elimu ya chuo kikuu kama Tanzania, kufukuza madaktari 200 waliosoma kwa wastani wa miaka 19 kila mmoja ni hasara kweli. Ngoja niweke tarakimu rahisi kabisa. Chukua miaka 7 ya shule ya msingi, halafu ongeza 6 ya sekondari, kisha ongeza mitano ya shahada ya kwanza ya udaktari na mwisho ongeza mwaka 1 wa mafunzo ya vitendo (Internship) inakupa jumla 19 kwa kila mmoja. Sasa ukizidisha miaka 19 kwa watu 200 unapata miaka 3,800 (Elfu tatu na mianane). Kwa hivyo miaka yote hii imepotea. Wakiamua kwenda kufanya kazi nchi nyingine, nchi hizo zitafaidi sana hiyo miaka 3,800 ya elimu. Kwamba walikuwa na haki ya kugoma au la ni mjadala mwingine. Leo nimejadili idadi ya miaka ya elimu itakayopotea kwa kufukuza madaktari 200.

Vyama Viendeshwe na wanachama

Ule uchaguzi wa mwaka jana umetoa funzo gani kwa vyama vinavyoitwa vya upinzani?( Sipendi hili neno upinzani; tuviiteje? Shindani?). Kwanza kabisa ingebidi wajifunze kwamba ruzuku haiwasaidii bali inawamaliza. Unajua ruzuku ndio inayofanya kila chama kitake kuweka mgombe wake ili angalau kipate mbunge na hatimaye ruzuku? Sisemi kwamba kuna vyama ambavyo vinaweka wagombea kwa sababu nyingine nje ya ruzuku. Ukiangalia kiundani kabisa ruzuku haifaidishi upinzani bali chama twawala. Katika ruzuku ya shilingi bilioni nane kwa mwaka CCM itaondoka na zaidi ya bilioni saba halafu kitakachobaki jamaa watagawana. Turudi kwenye hali halisi; ukitoa CCM ni chama gani kingine kinaweza kujigamba kwamba ruzuku inasaidia katika kampeni au katika kuimarisha chama? Ni asilimia ngapi kwa mfano ya fedha za kukodi helkopta ya CHADEMA ilitokana na ruzuku?

Ukweli ni kwamba kwanza kabisa chama ni kikundi cha watu wenye mwelekeo unaofanana au wanakubaliana kiitikadi. Kama ni kikundi basi inabidi kiendeshwe na hao wanachama. Hakuna haja ya kila mtanzania kuendelea kuendesha vyama ambavyo ni vya watanzania wachache sana. Hivi ni asilimia ngapi ya watanzania ni wanachama wa vyama vya siasa? Hili tulivalie njuga ili hii ruzuku ifutwe. Sioni kama eti ruzuku inasaidia kukuza vyama na hatimaye demokrasia. Kwanza hili suala la kufikiria demokrasia ni vyama vingi sijuhi limetoka wapi. Hata kama pesa hizi kinadharia zina lengo la kuimarisha vyama basi kinachoimarika ni kimoja tuu. Hata kama vingeimarika vyote, viimarishwe na wanachama wenyewe. Wanaopenda vyama wavichangie.

Hivi vyama vya upinzani ingebidi vianze kuchimba masuala ya msingi ambayo yanafanya CCM kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Kwa mfano mali ambazo CCM ilirithi wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Angalia viwanja vya mpira kibao bado ni vya CCM, majengo mengi ambayo yalijengwa kwa kodi za wananchi bado ni ya CCM. Kwa nini mali hizo ziendelee kubaki za CCM? Tume ya Nyalali ilipendekeza kwamba mali hizo zirudishwe Serikalini lakini mpaka leo hakuna kilichorudishwa. Halafu jamaa wa upinzani wanakaa kukimbilia ruzuku ambayo kila mwaka itaendelea kuongezeka kw CCM huku ikipungua kwao, huku Chama hiki twawala kikiendelea kufaidika na mapato ambayo ni mali ya kila mtanzania. Pamoja na mambo mengine ya katiba na tume huru ya uchaguzi mimi nimeongele mambo mawili yanayohusu pesa.

Hili la ruzuku wanablogu wote tulivalie njuga. Vyama viendeshwe na wanachama hizo hela za ruzuku zikabiliane na kipindupindu au shughuli nyingine za kimaendeleo.

Natamani Kipindupindu kifike Ikulu

Kuna mwanamuziki mmoja mtanzania, kati ya wale wanaoitwa wa kizazi kipya anatamani mambo ya kuchekesha sana katika moja ya nyimbo zake. Kwa mfano anatamani mlima Kilimanjaro uamie sijuhi wapi na bahari pia ihame. Mimi leo nakuwa kama yeye. Natamani Kipindupindu kilipuke Mikocheni, Osterbay, Masaki halafu kipige hodi Ikulu pia. Kila siku kinavamia Buguruni, Manzese na sehemu zingine za walalahoi. Hivi kweli tumeshindwa kabisa kudhibiti kipindupindu? Labda kikifika ikulu kitapatiwa ufumbuzi. Rais mpya kaanza kazi kwa kukaribishwa na mlipuko wa kipindupindu kama ilivyo kawaida ya kila mwaka. Sijuhi kama atakivalia njuga kwa Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu mpya au kitaendelea kumaliza watu kwa Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya? Kama waziri wa Afya ataendeleza mapambano ya magonjwa kwa warsha, semina na makongamano na kuchapisha fulana na kofia basi hakuna kitakachotokea. Safari hii Waziri wa Afya ni Profesa. Sijuhi kama atasadia lolote kwa sababu huko nyuma alishawahi kuwepo Profesa akaboronga pia. Mimi sijuhi aibu hii ya kipindupindu itaisha lini.

Nawajibika kuomba Radhi

Kwa kweli nimepotea bila kutoa maelezo kwanza. Naomba radhi kwa hilo Ndesanjo kataka kuunda tume pamoja na kutaka kuwasiliana na FBI nitafutwe. Nimerudi. Naanza na nukuu hii ya Frantz Fanon. Kwamba wananchi ndio nguvu ya kubadili mambo. Niliwahi kuizungumzia bila kuiweka nukuu yenyewe: “To educate the masses politically does not mean, cannot mean making a political speech. What it means is to try, relentlessly and passionately, to teach the masses that everything depends on them; that if we stagnate, it is their responsibility and that if we go forward it is due to them too, that there is no famous man or woman who will take responsibility for everything and the magic hands are finally only the hands of the people”. Frantz Fanon
Nimeiweka ili kusisitiza kwamba tuna wajibu wa kuelimisha na kwamba sisi pia ni wananchi ambao tunaweza kuleta mabadiliko.

Tuesday, January 03, 2006

Kimya wenzangu!

Jamani nimekuwa kimya kwa muda sasa. Nilikuwa nakusanya nguvu baada ya igizo la tarehe 14. Wale waliotarajia mabadiliko makubwa nadhani wamekata tamaa. Wengine wanasema bunge limerudia kuwa la chama kimoja. Lakini Frantz Fanon anasema tuendelee kuelimisha wananchi mpaka wajue wao ndio wenye nguvu ya kuleta mabadiliko na hakuna mtu yeyote mmoja anayeweza kuleta mabadiliko ya maana isipokuwa wao wenyewe. Kwa wale wanaokubaliana na kalenda Gregory basi kheri ya mwaka mpya.

KITABU CHA WAGENI