Tumepoteza maelfu ya miaka ya elimu
Hivi lile Sakata la kufukuzwa kwa madaktari limeishia wapi? Kama wote walifukuzwa basi ni kwamba taifa limepata hasara ya maelfu ya miaka iliyowekezwa kwenye elimu. Tunaambiwa kwamba, kila mwaka mmoja wa elimu mtu anaopata unaongeza ufanisi katika utendaji kazi ambao hutoa mchango katika ukuaji uchumi na kuongeza maslahi ya anayepata elimu hiyo. Kwa kifupi ni kwamba rasilimali watu ni mtaji mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi. Kwa nchi yenye watu wachache wenye elimu ya chuo kikuu kama Tanzania, kufukuza madaktari 200 waliosoma kwa wastani wa miaka 19 kila mmoja ni hasara kweli. Ngoja niweke tarakimu rahisi kabisa. Chukua miaka 7 ya shule ya msingi, halafu ongeza 6 ya sekondari, kisha ongeza mitano ya shahada ya kwanza ya udaktari na mwisho ongeza mwaka 1 wa mafunzo ya vitendo (Internship) inakupa jumla 19 kwa kila mmoja. Sasa ukizidisha miaka 19 kwa watu 200 unapata miaka 3,800 (Elfu tatu na mianane). Kwa hivyo miaka yote hii imepotea. Wakiamua kwenda kufanya kazi nchi nyingine, nchi hizo zitafaidi sana hiyo miaka 3,800 ya elimu. Kwamba walikuwa na haki ya kugoma au la ni mjadala mwingine. Leo nimejadili idadi ya miaka ya elimu itakayopotea kwa kufukuza madaktari 200.