Tuesday, May 16, 2006

Mkataba wa IPTL na sheria ya Takrima imetufunza nini?

Kwa wiki kadhaa sasa tumekuwa tukijadili na kufurahia sana kufutwa kwa sheria ya Takrima na Ile ya kumzuia mgombea binafsi. Lakini kuna uwezekano wa hawa jamaa wakarudi mahakama ya rufaa kukatia rufaa rushwa. Pia tumeisoma taarifa jinsi tulivyoingizwa pabaya na Wamalasia na Watanzania wenye uroho wa pesa kwenye mkataba wa IPTL. Inabidi katika mviringo wetu wa Blogu pamoja na kwenye magazeti tuanze kujadili kwa kina kabisa baadhi ya wahusika ili jamii iwajue. Kwa mfano; Andrew Chenge, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Serikali ametajwa kama mhusika mkubwa sana kwenye IPTL. Alihusika kwa mambo mawili; kwanza kama mwanasheria mkuu wa Serikali ofisi yake inahusika na kutoa ushauri kwa serikali kwa mambo yote ya kisheria; lakini la pili ni kwamba alikuwa kikwazo katika kutoa pingamizi la kukamatwa kwa Rwegamarila ashitakiwe kwa rushwa kwa kudai hakuna ushaidi.
Hakuna ubishi kwamba Chenge na ofisi yake ni mhusika na Mhandisi wa Sheria ya Takrima. Alikuwa anaitetea kweli. Wakati mwingine alikuwa akiwatukana wabunge waliokuwa wakihoji hiyo sheria. Ni kweli kwamba sheria hiyo imemsaidia kuingia tena bungeni sasa. Jamani mtu huyu tena kapewa wizara ya Afrika mashariki. Hii ni wizara ambayo inahitaji umakini mno. Tunaongelea ushirikiano na baadaye shirikisho. Katika kipindi cha Mpito kutakuwa na makumi ya mikataba. Chenge anaweza kuisimamia?
Chenge na ofisi yake pia wanahusika na mikataba yote mibovu ambayo sasa Serikali inakiri kwamba itarekjelewa upya. Sasa sijuhi kama atatuvusha katika jahazi hili la ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni lazima mambo haya yavaliwe njuga.

Sunday, May 14, 2006

Kina Galileo wasingehoji tungekuwa wapi?

Ndani ya blogu hii kuna habari ya Askofu kuzaa mtoto na kujificha. Hoja hiyo imejadiliwa sana. Baadhi ya watoa maoni wanaonyesha ni jinsi gani wanavyotaka mawazo mgando yaendelee. Hasa yale yahusuyo imani. Hivi kama kina Galileo wa Galileo hawakuhoji baadhi ya mambo bado leo tungeambiwa dunia ni mstatili na jua linazunguka toka mashariki kwenda magharibi? Kama hawakubali adhabu ya kifo kwaa kuhoji leo tungekuwa wapi? Nimeamua kuweka hapa chini maoni ya mmoja wa wachangiajia ambaye hataki watu wahoji uhalali wa papa anayeongoza watu zaidi ya bilioni moja kuchaguliwa na wazee wanaume wasiozidi mia moja. soma sehemu ya maoni hayo hapa chini.
"Nakumbuka uliwahi kuandika katika gazeti la Rai ukihoji uhalali wa uchaguzi wa Baba Mtakatifu anaye chaguliwa na Makardinali na kuongoza kanisa zima! Wewe ni Padri mkatoriki unaye hoji uhalari wa Baba Mtakatifu?! Zaidi umehoji ukweli wa mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu utumiaji wa Kondomu. Kama "Padri" wa kwanza mkatoriki umeunga mkono matumizi ya Kondomu, kama kinga dhidi ya Gonjwa hatari la Ukimwi.Haya yote yamekupatia sifa katika ulimwengu unaopinga msimamo wa Kanisa katoliki katika masulala mbalimbali yanayo husu maadili"
Mambo sasa yameanza kubadilika. Huko Uchina wamebariki maaskofu katoliki bila mkono wa Vatican. Wametolewa macho lakini wachina wameendelea. Huko Marekani wamemkabidhi uaskofu mtu aliyeoa. Sasa hapo ndipo utaona watu wameanza kuhoji na kutekeleza mambo ambayo awali yalikuwa mwiko kuyahoji. Miaka ya sitini Mwanaharakati Malcom X, katika moja ya hotuba zake alisifia sana Uchina kwa kuwa nchi ambayo ilikuwa ikifanya maamuzai yake mengi bila kuwasikiliza mabwana wa magharibi na mavyombo yao yanayoitwa UN, Benki ya Dunia, IMF nakadhalika. Alibashiri kwamba China ingeendelea sana. Sote tunaona yanayotokea China. Sasa wameanza kuchoka na kutawaliwa na Vatican. Baada ya kukubali dini za kigeni kwa mbinde sana sasa wameanza kujichukulia maamuzi yao wenyewe. Wacha watu wahoji. Kama watu wasingehoji basi tungekuwa mbali sana.

KITABU CHA WAGENI