Mkataba wa IPTL na sheria ya Takrima imetufunza nini?
Kwa wiki kadhaa sasa tumekuwa tukijadili na kufurahia sana kufutwa kwa sheria ya Takrima na Ile ya kumzuia mgombea binafsi. Lakini kuna uwezekano wa hawa jamaa wakarudi mahakama ya rufaa kukatia rufaa rushwa. Pia tumeisoma taarifa jinsi tulivyoingizwa pabaya na Wamalasia na Watanzania wenye uroho wa pesa kwenye mkataba wa IPTL. Inabidi katika mviringo wetu wa Blogu pamoja na kwenye magazeti tuanze kujadili kwa kina kabisa baadhi ya wahusika ili jamii iwajue. Kwa mfano; Andrew Chenge, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Serikali ametajwa kama mhusika mkubwa sana kwenye IPTL. Alihusika kwa mambo mawili; kwanza kama mwanasheria mkuu wa Serikali ofisi yake inahusika na kutoa ushauri kwa serikali kwa mambo yote ya kisheria; lakini la pili ni kwamba alikuwa kikwazo katika kutoa pingamizi la kukamatwa kwa Rwegamarila ashitakiwe kwa rushwa kwa kudai hakuna ushaidi.
Hakuna ubishi kwamba Chenge na ofisi yake ni mhusika na Mhandisi wa Sheria ya Takrima. Alikuwa anaitetea kweli. Wakati mwingine alikuwa akiwatukana wabunge waliokuwa wakihoji hiyo sheria. Ni kweli kwamba sheria hiyo imemsaidia kuingia tena bungeni sasa. Jamani mtu huyu tena kapewa wizara ya Afrika mashariki. Hii ni wizara ambayo inahitaji umakini mno. Tunaongelea ushirikiano na baadaye shirikisho. Katika kipindi cha Mpito kutakuwa na makumi ya mikataba. Chenge anaweza kuisimamia?
Chenge na ofisi yake pia wanahusika na mikataba yote mibovu ambayo sasa Serikali inakiri kwamba itarekjelewa upya. Sasa sijuhi kama atatuvusha katika jahazi hili la ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni lazima mambo haya yavaliwe njuga.