Tuesday, June 12, 2007

Askofu agawa kondomu

Alhamisi ya tarehe 7 Juni 2007, BBC ilirusha kipindi cha Hard Talk ambapo mwandishi maarufu Steven Suckur alifanya mahojiano na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Rusternburg Nchini Afrika ya Kusini. Askofu huyo, Kevin Dowling alikiri kugawa kondomu kwa watu ili wajikinge na maambukizi ya UKIMWI. Alisema kwamba yeye kama askofu ameshuhudia mengi, anaona watu wakifa ambapo pengine wangestahili kupona. Alisema katika moja ya kliniki sehemu hizo, asilimia 50 ya wanawake wanaohudhuria kliniki ya wajawazito wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Wengi wa wanaothirika ni wahamiaji masikini kutoka katika majimbo yenye hali mbaya sana kimaisha hase jimbo la Eastern Cape. Baadhi ya wahamiaji hao huja kutafuta namna ya kujikwamua kimaisha katika maeneo hayo ambapo kuna mgodi wa madini, lakini wengi hasa wanawake hujikuta wakijihusisha na ngono kama njia ya kujikimu baada ya kukuta hakuna cha kufanya.

Alipoulizwa kama haoni huku ni kupingana na Vatican, Askofu huyo ambaye pia alikuwa mmoja wa wapambanaji wa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini humo alisema ni kweli mtazamo wa kanisa si huo lakini yeye anaangalia hali halisi na mazingira aliyomo. Anasema akiwatembelea watu katika maeneo hayo wanaoishi kwenye vibanda vibovu kabisa anawakuta wengi wakiwa katika hali mbaya sana jambo linalomfanya ahisi kwamba wangeweza kupona kama wangejikinga. Hilo linamsukuma kuwagawia kondomu watu wengi ili kuponya maisha yao na madhara yanayoambatana na UKIMWI. Anaendelea kusema kuwa watu anaowahudumia si wakatoliki tu bali ni kutoka katika dini na madhehebu mbalimbali na kwamba anachofanya ni kujaribu kuwasaidia watu kutua mizigo na si kuwatwisha kama neno la bwana linavyonena!

Askofu agawa kondomu

Alhamisi ya tarehe 7 Juni 2007, BBC ilirusha kipindi cha Hard Talk ambapo mwandishi maarufu Steven Suckur alifanya mahojiano na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Rusternburg Nchini Afrika ya Kusini. Askofu huyo, Kevin Dowlin alikiri kugawa kondomu kwa watu ili wajikinge na maambukizi ya UKIMWI. Alisema kwamba yeye kama askofu ameshuhudia mengi, anaona watu wakifa ambapo pengine wangestahili kupona. Alisema katika moja ya kliniki sehemu hizo, asilimia 50 ya wanawake wanaohudhuria kliniki ya wajawazito wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Wengi wa wanaothirika ni wahamiaji masikini kutoka katika majimbo yenye hali mbaya sana kimaisha hase jimbo la Eastern Cape. Baadhi ya wahamiaji hao huja kutafuta namna ya kujikwamua kimaisha katika maeneo hayo ambapo kuna mgodi wa madini, lakini wengi hasa wanawake hujikuta wakijihusisha na ngono kama njia ya kujikimu baada ya kukuta hakuna cha kufanya.

Alipoulizwa kama haoni huku ni kupingana na Vatican, Askofu huyo ambaye pia alikuwa mmoja wa wapambanaji wa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini humo alisema ni kweli mtazamo wa kanisa si huo lakini yeye anaangalia hali halisi na mazingira aliyomo. Anasema akiwatembelea watu katika maeneo hayo wanaoishi kwenye vibanda vibovu kabisa anawakuta wengi wakiwa katika hali mbaya sana jambo linalomfanya ahisi kwamba wangeweza kupona kama wangejikinga. Hilo linamsukuma kuwagawia kondomu watu wengi ili kuponya maisha yao na madhara yanayoambatana na UKIMWI. Anaendelea kusema kuwa watu anaowahudumia si wakatoliki tu bali ni kutoka katika dini na madhehebu mbalimbali na kwamba anachofanya ni kujaribu kuwasaidia watu kutua mizigo na si kuwatwisha kama neno la bwana linavyonena!

Wednesday, June 06, 2007

Paper ya padre Karugendo

Padre Karugendo hivi karibuni alitoa mada kuhusu kujikinga na UKIMWI katika usharika wa Chuo Kikuu DSM. Naiweka hapa ili uisome.
KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA UKIMWI

Waheshimiwa mabibi na mabwana. Bwana asifiwe!
Tuombe:
Tumwombe Mungu Mwenyezi muweza wa yote,
Muumba wa Mbingu na Dunia,
Mwenye wingi wa upendo, huruma na hekima,
Mwenye kujali na kusamehe,
Anayetujalia Uhai,uhuru na utashi,
Anayetufunulia kila kitu mpaka kututumia
Mwanaye wa pekee kuja kutukomboa;
Atushushie roho wake Mtakatifu,
Aje kutuongoza katika maongezi yetu ya leo.
Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu. Amen!

Ninawashukuru sana kunikaribisha katika Usharika wenu wa Chuo Kikuu, ili tuweze kushirikiana katika kujadili na kuelimishana juu ya ugonjwa hatari wa UKIMWI.

Katika maongezi yangu nitaongozwa na masomo matatu:

“Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na atapata malisho. Mwizi huja kwa sababu ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima- uzima kamili” ( Yohana 10:9).

2. “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yohana 5: 26).

3. “Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” (Yohana 17:21)

UKIMWI, ni somo pana sana na linagusa nyanja zote katika maisha yetu. Hivyo kuna mambo mengi ya kujadili juu ya ugonjwa huu. Mengi yamejadiliwa na bado mijadala inaendelea na ndiyo maana tuko hapa siku ya leo. Imani yangu ni kwamba kwa vile hapa ni sehemu ya wasomi. Mijadala kama Ukimwi ni nini, Virusi vya Ukimwi ni nini, Ukimwi ulianzia wapi, Ukimwi unaambukiza kwa njia zipi, njia za kujikinga,dawa za kurefusha maisha na utata mwingi unaozunguka ugonjwa huu si mipya. Na kwa vile kuna wachangiaji wengine, basi niwaombe niongelee kipengele kimoja: Kujikinga na Maambukizi ya UKIMWI. Nikiwa na lengo la kusisitiza wajibu wetu wakristu wa kulinda na kuutunza uhai. Kama anavyosema Bwana wetu Yesu kristu: “Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima- uzima kamili.”

UKIMWI, unaambukiza kwa njia mbali mbali. Nafikiri na hili si geni kwenu. Nawaomba niongelee njia moja tu inayosambaza ugonjwa huu kwa asilimia kubwa: Ngono.

Sintaingia kwenye upande wa Ushoga na Usagaji. Nitajikita kwenye kujamiana katika hali ya kawaida inayokubalika katika jamii na katika kanisa.

Wataalamu wa jambo hili la kujingina na maambukizi ya Ukimwi (Ngono), wanapendekeza njia kama tatu. Padri Joinet, ambaye amekuwa mstari wa mbele,katika swala hili la kujikingia na maambukizo ya Ukimwi, anaoegelea mashua tatu. Yeye anauchukulia UKIMWI, kama mafuriko – na kwamba watu wanatafuta namna ya kuokoa maisha yao kwa kuyakimbia mafuriko. Mashua hizi tatu ni:
Uaminifu
Kujinyima
Kondomu.

Yeye anasema kwa vile mtu ana uhuru na utashi, na kwa vile kuna njia tatu za kujikinga – hakuna haja ya kupoteza maisha. Mashua zote ni salama, hivyo kila mtu anaweza kujiponya kwa kuchagua mashua mojawapo. Na anasema mambo kama yakikwendea vibaya kwenye mashua moja, basi mtu unaweza kuamua kuhamia kwenye mashua nyingine. Anasema ni uzembe na kutojali mtu kufa kwa mafuriko wakati mashua zipo. Ni zaidi ya miaka 15, Fr. Joinet, akihubiri juu ya mashua tatu, lakini maambukizi ya virusi vya UKIMWI bado yanashika kasi ya kutisha. Maana yake ni kwamba, kuna baadhi ya watu wanaamua kufa kwa mafuriko kuliko kuingia kwenye mashua mojawapo!

Wengine kama Mheshimiwa Askofu Gamanywa, wanaongelea kitu kilekile, lakini kwa mtanzamo mwingine na kwa kukwepa Kondomu;
Subiri
Tosheka naye
Acha kabisa.

Njia hizi nazo ni salama kabisa. Lakini la kushangaza, ni kwamba maambukizi ya UKIMWI, yanapanda badala ya kushuka. Maeneo mengine yanashuka kidogo – lakini kwa wastani hapa Tanzania maabukizi ya virusi vya UKIWMI bado yako juu.

Kwa sabablu zilizojuu ya uwezo wangu, ninawaomba niongelee njia mbili tu:
Uaminifu
Kondomu.

Maana hizi nyingine:
Kujinyima
Acha kabisa.

Ni za watu wachache sana ambao ninafikiri hawaishi katika dunia yetu hii. Hizi ni za wateule wachache. Nafikiri sisi tunatafuta njia za kuwakinga watu wengi, jamii nzima. Hivyo hizi za wateule wachache hazitusaidii sana.

Uaminifu.

Kile ambacho Padri Joinet, anakiita Mashua ya Uaminifu, ndicho Askofu Gamanywa na viongozi wengine wa dini wanakiita Tosheka naye. Maana yake ni kwamba mtu awe na mpenzi mmoja. Mme mmoja, mke mmoja! Kwa kuzuia maambukizi ya UKIMWI, hii ni njia nzuri kuliko zote!

Jambo hili si jipya katika kanisa. Ndoa ya kikristu ni ya mme mmoja, mmke mmoja. Hiyo ndiyo maana ya tosheka naye. Kwenda kinyume ni kuvunja uaminifu.

Sote tumekwisha shuhudia ndoa za Kikristu zinazofunjika, tumeshuhudia wakristu wenye wanawake zaidi ya wawili, tumeshuhudia nyumba ndogo, tumeshuhudia watoto wanaozaliwa nje ya ndoa nk. Nisingependa kuingia sana katika jambo hili. Kitu ninachopenda kujadiliana na nyinyi ni je:
Kuna Uaminifu katika ndoa za Kikristu?
Uaminifu ni kitu kinachowezekana katika ndoa na katika mapenzi?
Maana kama Uaminifu ni njia nzuri ya kujikinga maabukizi ya Ukimwi, ni bora tukahakikisha kama kweli njia hii ni salama, vinginevyo tunajiingiza katika hatari.



Mfano:

Mimi ni Padri wa Kanisa Katoliki. Sisi wakatoliki tuna kitu kinachoitwa Sakramenti ya kitubio. Waumini wanatubu dhambi zao kwa Padri. Sina lengo na kutaja dhambi za watu. Ninautumia huu kama mfano wa kutusaidia. Kwa kipindi cha miaka 18, niliyoungamisha, sikukutana na familia hata moja yenye Uaminifu katika ndoa. Sikukutana na mtu hata mmoja, mwenye uaminifu katika mapenzi:

Kwa maana kwamba kila mtu mwenye ndoa niliyemuungamisha, alitaja dhambi ya kuzini na kutembea nje ya ndoa!

Kwa maana kwamba kila mtu mwenye mpenzi niliyemuungamisha, alitaja dhambi ya kukosa uaminifu kwa mpenzi wake.

Nimeishi Ulaya, nimeungamisha, hali ilikuwa hivyo hivyo. Nimeishi Mbeya, nimeugamisha, hali ilikuwa hivyo hivyo. Nimeishi Karagwe, nimeungamisha, hali ilikuwa hivyo hivyo. Ninataja sehemu mbali mbali ili isije ikachukuliwa kwamba tabia ya kutokuwa na uaminifu katika ndoa na mapenzi ni ya sehemu Fulani.

Nimekaa kwenye parokia moja ya Bushagaro Karagwe, kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Kipindi chote hicho nimeshuhudia watu wakifa kwa UKIMWI. Watu niliowafahamu, niliowaungamisha, watu tuliokuwa tukisali pamoja. Kwa kipindi chote hicho nimeshuhudia watu walio kwenye ndoa na wenye wapenzi wakiungama dhambi ya kuzini. Na kipindi hicho UKIMWI, ulikuwa unapamba moto.

Mapadri haturuhusiwi kutaja au kutumia maungamo kwa namna yoyote ile. Hata kama unajua kwamba aliyeungama ametembea na mtu mwenye virusi, wakati amemwacha mke wake nyumbani, unakaa kimya. Badala ya kutetea Uhai, unabariki kifo!

Je, katika hali kama hii tunaweza kusema kwamba uaminifu ni njia ya kukinga maambukizi ya Ukimwi? Labda tatizo la kutokuwa na uaminifu katika ndoa ni la wakatoliki peke yao? Inawezekana kwenu nyinyi Walutheri ni tofauti? Nafikiri nitakuwa nimechokaza majadiliano.

Mwaka 2002, niliamua kukataa kubariki vifo na kuanza kutetea uhai kwa nguvu zangu zote.Nilivunja ukimya na kuwashawishi waumini kuuvunja ukimya ili tushirikiane kwa pamoja kupambana na maambukizi ya UKIMWI. Niliunga mkono matumizi ya kondomu. Katika mkutano wa “National Multisectoral Aids Conference” nilitoa mada na kuwaomba waheshimiwa Maaskofu kuvunja ukimya. Maana kama kuna watu wenye ushuhuda kwamba uaminifu katika ndoa ni kitu kigumu ni mapadri wa kanisa Katoliki. Niliwaomba maaskofu kama hawapendi kuunga mkono matumizi ya kondomu, basi wanyamaze. Au waendeshe kampeni ya chini kwa chini. Maana maaskofu wana ushawishi mkubwa, wakisema kondomu ni dhambi, watu wanafuata hata bila ya kufikiri kwanza.Jambo hili liliniingiza matatani na uongozi wa Kanisa katoliki hadi leo hii.

Ukweli ndo huo, kwamba hadi leo hii Mapadri tunaendelea kuchochea maambukizi ya Ukimwi. Watu wanaungama kuzini, tunawabariki na kuwasafisha. Wanarudi kuzini – wakirudi tunawabariki na kuwasafisha. Ni mzuguko usiokuwa na mwisho. Tunabariki vifo, badala ya kubariki uhai! Na kwa nguvu zote tunaendelea kuhubiri kwamba njia pekee ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni uaminifu na Tosheka naye. Nitakuwa nimechochea majadiliano zaidi?





KONDOMU.


Wataalamu wanasema Kondomu, ikitumiwa vizuri ina uwezo wa kuzuia maambukizi kwa asilimia 98. Kuna mabishano mengi juu ya Kondomu. Wengine wanasema virusi vinapita. Wengine wanatoa ushahidi wa watu waliotumia Kondomu, wakapata maambukizi. Wengine wanasema kwamba Kondomu,ni biashara. Yako mabishano mengi. Nisingependa kujiingiza sana kwenye mabishano hayo. Labda moja tu kwa wale wanaosema kwamba Kondomu inachochea uzinzi. Ninakataa kukubaliana na watu hawa:

Kondomu ni silaha. Na kawaida mtu kuwa na silaha, si kigezo cha kuitumia hiyo silaha vibaya. Benki zetu masaa yote zinalindwa na mapolisi wenye bunduki zenye risasi. Ni mara ngapi mapolisi hawa wanafyatua risasi ovyo? Zinatumika pale yanapotokea majambazi.







Yapo mambo mengi yanayochochea uzinzi:
Pombe,
Madawa ya kulevya.
Mavazi yasiyokuwa ya heshima,
Picha za ngono katika Internet,
Umaskini,
Ujinga nk.

Hadi leo hii jamii yetu haijafanikiwa kuwa na mfumo mzuri wa kupambana na hayo niliyoyataja. Baadhi ya waandishi wameandika makala, riwaya, michezo ya kuiigiza na mashairi kuonyesha kwamba niliyoyataja hapo juu yanachochea uzinzi. Mkipata nafasi mnaweza kujisomea vitabu kama:
Kisiki Kikavu- Dkt.Aldin Mutembei.
Ua la Faraja- William Mkufya
Mpe Maneno Yake- Freddy Macha.

Kwanini kanisa linapiga vita matumizi ya Kondomu?

Kwenye karne ya tatu kanisa lilishambuliwa na falsafa ya Kigriki. Falsafa ya akina Aristotle na Plato. Hawa walianzisha mfumo wa kufikiri uliokuwa unatenga vitu vyote katika makundi mawili:
Matter
Spirit.

Matter, ni vitu vyote vinavyokufa kama mwili. Na spirit ni vitu vyote vinavyodumu kama roho. Kwa maoni yao vitu vinavyokufa (Matter) vilikuwa vitu vichafu, dhambi nk. Lakini vile vinavyodumu (Spirit) vilikuwa vitakatifu.

Falsafa hii iliuchukulia mwili na matendo yote ya mwili kama ngono kuwa ni machafu, ni dhambi. Mtu aliyetaka kuishi maisha ya kitakatifu, ilibidi aachane na matendo ya mwili.

Hata kwa watu wenye ndoa, ngono iliruhusiwa pale ilipokuwa inalenga kutunga mimba. Ili kushika utakatifu, watu walishauriwa kufanya tendo hilo bila kulifurahia.

Watu kama Pliny, walifikia hatua ya kuisifia tembo, maana ilikuwa ikiingia kwenye joto mara moja baada ya miaka miwili. Origen, aliamua kujihasi ili asifanye ngono na Plotinus, aliishi maisha yake yote akiona aibu kuwa na mwili.

Lakini mtu aliyeingiza chuki ya furaha ya tendo la ngono katika kanisa ni Mtakatifu Augustine (430). Huyu aliunganisha dhambi ya asili na furaha ya tendo la ngono. Alisisitiza kwamba ni lazima mbegu za uzazi zidondoke kwenye sehemu yake na ziwe zinalenga kutunga mimba. Mafundiso haya yaliwageuza wanawake kama vyombo vya uzazi – yaliwanyima haki ya kufurahia tendo la ngono na kuwa na haki sawa katika jamii. Mafundisho ya kanisa juu ya ndoa hadi leo hii yanafuata mafunfisho ya Mtakatifu Augustine.

Mwandishi Uta Ranke- Heinemann, wa Ujerumani katika kitabu chake cha Eunuchs For The Kingdom of Heaven, anatwambia kwamba Mtakatifu Thomas Aquinas, alifikiri kwamba kumwaga mbegu za kiuume kwenye nafasi tofauti ni dhambi kubwa kuliko mtu kufanya ngono na mama yake mzazi!

Msingi huu ndio unalifanya kanisa kupinga matumizi ya Kondomu, maana ukitumia kondomu, mbegu zinamwagika kwenye mpira na zinakuwa hazilengi kutunga mimba.

Enzi tulizomo hakuna mtu ambaye bado anaamini kwamba kila tendo la ngono ni lazima lilenge kutunga mimba. Hata Kanisa lo limepiga hatua na kuongeza kwamba mbali na kutunga mimba, tendo la ndoa ni muhimu katika kuimarisha na kuchochea mapenzi katika ndoa. Ila kwa vile kanisa linapinga uzazi wa mpango, linaendelea kupinga matumizi ya Kondomu.

Hoja na chamgamoto iliyombele yetu na mbele ya kanisa, ni kwamba hatuongelei juu ya kudondosha mbegu kwenye mpira au kufanya uzazi wa mpango. Tunaongelea juu ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya UKIMWI. Ugonjwa ambao umepoteza mamilioni ya watu. Hivyo tunaongea juu ya kuulinda uhai.

HITIMISHO:

Kwa kuhitimisha, ningeomba kusema hivi: Ukiniuliza swali la haraka juu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwenye kongamano au semina. Jibu langu litakuwa kwamba kinga ya kwanza ni Uaminifu, na kinga ya pili ambayo inaaminika zaidi ni Kondomu. Lakini ukiniuliza swali hilo hilo tukiwa tumekaa na kujadiliana kama tunavyofanya leo, kwenye jumuiya ya waumini, jibu langu litakuwa tofauti.

Nitakujibu hivi: Kinga pekee ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, ni kubadilisha mfumo wa jumuiya zetu za kikristu, ni kubadilisha mfumo wa familia zetu ni mtu binafsi kubadilisha mfumo wake wa maisha.

Njia pekee ya kukinga maambukizi ya virusi vya Ukimwi, magonjwa mengine ya hatari na kukinga majanga mengine kama umasikini, ujinga, vita na upweke, ni kujenga jumuiya zinazoishi Utatu: Mungu Baba, Mungu Mwana Na Mungu Roho Mtakatifu. Ni kujenga familia zinazoishi utatu. Ni kila mtu kuishi maisha ya Utatu.

Kinga pekee ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, ni kujenga jumuiya zinazojaliana, zinazojuliana hali, zinazochungana, zinazolindana na zinazowajibishana.

Jumuiya za Kikristu tulizonazo sasa hivi, familia za kikristu tulizonazo sasa hivi, ambazo zinatishiwa na ugonjwa wa Ukimwi na hatari nyinginezo, ni zile ambazo kila mtu yuko kivyake.Hakuna anayemchunga mwenzake, hakuna anayemlinda mwenzake na hakuna anayemwajibisha mwenzake. Kila mtu amejifungia katika nafsi yake:

Hakuna uwazi katika familia,
Hakuna kufunuliana katika familia,
Hakuna kushirikishana katika familia,
Hakuna kuchukuliana katika familia,
Hakuna kulindana na kuchungana katika familia.

Hivyo hivyo hakuna uwazi katika jumuiya zetu,
Hakuna kufunuliana katika jumuiya zetu,
Hakuna kushirikishana katika jumuiya zetu,
Hakuna kuchukuliana katika jumuiya zetu,
Hakuna kulindana na kuchungana katika jumuiya zetu.

Kila mtu anaufunga moyo wake na kubaki na siri nyingi ndani ya nafsi yake. Hata na mambo ya kawaida kama vile kupenda yanafanywa siri. Mambo kama tamaa, uchu, furaha,uzuni nk, yanabaki siri ndani ya moyo wa mtu. Kuna waandishi wengi, mfano kama Elieshi Lema (Parched Earth) wameandika juu ya ya tabia hii ya mtu kujifunga ndani ya nafsi yake. Mkipata nafasi mnaweza kujisomea vitabu hivyo kikiwemo cha “Parched Earth”. Mtu anayeufunga moyo wake hawezi kufanikiwa kutengeneza familia ya kuishi Utatu. Na kama hakuna familia za kutengeneza utatu, ni vigumu kuwa na Jumuiya zenye kuishi utatu.

Bila kuwa na Jumuiya zenye kuishi utatu, ni lazima tuandamwe na majanga mengi. Si Ukimwi peke yake. Leo tunaongelea UKIMWI, lakini kesho na keshokutwa yatakuja majanga mengine katika jamii yetu. Ni lazima tuwe na mfumo imara na wa kudumu kuweza kuyakabili majanga yanayoweza kutukumba kimwili na kiroho.


Bwana wetu Yesu anasema hivi:

“Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” ( Yohana 17: 21.

Maneno haya ya Yesu, yanaeleweka vizuri ukiyaunganisha na yale ya Yohana 5: 19-20.

“Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya baba, Mwana hukifanya vile vle. Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe,tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu”.

Yesu, alikuwa akielezea uhusiano wake na Mungu Baba. Jinsi yalivyo maisha ya uwazi. Hakuna siri kati yao. Analolijua Mungu Baba, analijua Mungu Mwana, na analijua Mungu roho mtakatifu. Hii ndiyo maana ya Mwana kuwa ndani ya Baba na Baba kuwa ndani ya Mwana na wote wawili kuwa ndani ya Roho Mtakatifu. Wanaishi maisha ya utatu, katika uwazi na kufunuliana. Uwazi huu unawafanya waungane na kuwa kitu kimoja.







Yesu, anatuombea na sisi kuishi maisha ya Utatu. Kuishi maisha ya uwazi. Tuwe ndani ya Yesu, nay eye awe ndani yetu na sote tuwe ndani ya Baba. Tuwe na familia zenye kuishi utatu. Baba ndani ya familia amjue mama, na mama amjue Baba. Baba ajifunue kwa mama, na mama ajifunue kwa Baba. Hata kama baba anavutiwa na mwanamke mwingine, au mama anavutiwa na mwanaume mwingine, wafunuliane! Kwa njia hii wanaweza kulindana, kuchungana, kuchukuliana na kusaidiana. Ni katika uwazi na kufunuliana familia inaweza kuungana na kuwa kitu kimoja.

Baba na mama wakichukuliana, wakafunuliana, wakalindana na kuchungana, wanajenga mfumo wa kuwalinda na kuwachunga watoto wao. Watoto watakua katika uwazi na kutembea katika mwanga. Watafundishwa maadili mema bila ya matatizo na kuwa sehemu ya familia inayoishi utatu.

Familia zilizoungana na kuwa kitu kimoja, zinatengeneza jumuiya iliyoungana na kuwa kitu kimoja. Jumuiya ikiungana na kuwa kitu kimoja, ni lazima pawepo kufunuliana, kujaliana, kulindana, kuchungana na kusaidiana.

Jumuiya inayoishi Utatu, ndiyo inayoweza kupambana na majanga makubwa kama UKIMWI. Kwa ufafanuzi zaidi juu ya Jumuiya inayoishi Utatu mnaweza kujisomea kitabu cha Marehemu Askofu Christopher Mwoleka: “The Church as a Family”

Yote niliyoyasema yanawezekana pale tu ambapo kila mmoja wetu, kila mwanausharika na kila mtanzania, atasali sala kama ile ya Bwana Sufi Bayazid:

“Nilipokuwa kijana mwanamapinduzi, sala yangu pekee kwa Mungu ilikuwa: ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kuubadilisha ulimwengu’

“Nilipofikisha umri wa mtu mzima na kugundua kwamba sijafanikiwa kuibadilisha roho hata moja, nilibadilisha sala: ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kuwabadilisha watu wanaonizunguka, familia yangu na marafiki zangu’

“Sasa ninapozeeka, bila kufanikiwa kuubadilisha ulimwengu sala yangu imekuwa: ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kujibadilisha mimi mwenyewe’

“Kumbe ningesali hivi tangia mwanzo, nisingepoteza muda wangu bure” (The Song of the Bird – uk 153 – tafsiri ni yangu).





Kama anavyosema Sufi Bayazid, tusiweke nguvu nyingi katika kutaka kuyabadilisha maisha ya wengine, kabla ya kubadilisha maisha yetu sisi wenyewe. Hivyo basi kinga pekee ya kusambaa kwa virusi vya Ukimwi, ni kila mmoja wetu kubadilisha maisha yake mwenyewe. Ni kila mmoja wetu kujinyoshea kidole. Kwa njia hii tunaweza kuulinda na kuutetea uhai!

Kristu yu hai, jana, leo, kesho na hata Milele.

Asante sana kunisikiliza.

Na,
Padri Privatus Karugendo
e-mail:pkarugendo@yahoo.com




Marejeo:

Agano jipya – injili ya Yohana.
Kisiki Kikavu- Dkt Aldin Mutembei
Ua la Faraja- W-Mkufya
The Song of the Bird – Anthony de Mello
AIDS-Petit Echo- Fr.Bernard Joinet.
Eunuchs For The Kingdom of Heaven,1991.- Uta Ranke-Heinemann
HIV/AIDS Challenges for Professionals- Fr.Privatus Karugendo, 2002
The Church as a Family- Late Bishop Christopher Mwoleka.
Mpe Maneno Yake- Freddy Macha.
Parched Earth – Elieshi Lema.

Natia jembe Mpini

Nimekuwa kimya muda mrefu na niliondoka bila kuaga. Sasa narejea, nasema natia jembe mpini nirudie kazi yangu. Naendlea na kublog sasa. Samahani kwa kupotea bila taarifa

KITABU CHA WAGENI